Je, roho zinakufa au ni wiliwili tu ndio inakufa? Kuna maoni tofauti katika suala hili. Kuna wenye kusema kuwa roho zinakuwua kwa sababu ni nafsi na kila nafsi itaonja mauti. Wametumia dalili maneno ya Allaah:

وَيَبْقَىٰ وَجْهُ رَبِّكَ ذُو الْجَلَالِ وَالْإِكْرَامِ

“Utabakia Uso wa Mola wako wenye utukufu na ukarimu.” 55:27

كُلُّ شَيْءٍ هَالِكٌ إِلَّا وَجْهَهُ

“Kila kitu ni chenye kuangamia isipokuwa Uso Wake.” 28:88

كُلُّ نَفْسٍ ذَائِقَةُ الْمَوْتِ

”Kila nafsi itaonja mauti.” 03:185

Wanasema kuwa ikiwa Malaika wanakufa basi nafsi za wanaadamu zina haki zaidi ya kufa. Allaah (Ta´ala) amesema kuhusu watu wa Motoni:

قَالُوا رَبَّنَا أَمَتَّنَا اثْنَتَيْنِ وَأَحْيَيْتَنَا اثْنَتَيْنِ

“Watasema: “Mola wetu! Umetufisha mara mbili na Umetuhuisha mara mbili.” 40:11

Mauti ya kwanza yanahusiana na viwiliwili na ya pili yanahusiana na roho.

Wengine wakasema kuwa roho hazifi na kwamba zimeumbwa kwa ajili ya kubaki. Kwa mujibu wao wanaonelea kuwa viwiliwili ndio hufa. Wametumia dalili zile Hadiyth zinazofahamisha kuwa roho zinaneemeshwa na kuadhibiwa pale zinapotengana na kiwiliwili mpaka pale Allaah atapozirejesha kwenye viwiliwili vyake. Roho zikifa basi neema na adhabu vitakatika. Allaah (Ta´ala) amesema:

وَلَا تَحْسَبَنَّ الَّذِينَ قُتِلُوا فِي سَبِيلِ اللَّـهِ أَمْوَاتًا ۚ بَلْ أَحْيَاءٌ عِندَ رَبِّهِمْ يُرْزَقُونَ

“Na wala usiwadhanie wale waliouawa katika njia ya Allaah wamekufa. Bali wahai kwa Mola wao wanaruzukiwa.” 03:169

Amesema hivo pamoja na kuwa roho zao kwa kukata kabisa zimetengana na viwiliwili vyao vilivyokufa. ´Allaamah Ibn-ul-Qayyim amesema:

“Maoni sahihi ni kwamba nafsi zinakuwa pale zinapotengana na kuachana na viwiliwili vyao. Ikiwa haya ndio yanayokusudiwa kunaposemwa kuwa zinakufa, basi ni kweli kwamba zinaonja mauti. Na ikiwa kunakusudiwa kuwa zinapotea na kutokuwepo kabisa kabisa, basi hazifi. Bali ni zenye kubaki baada ya kuumbwa. Ima zinakuwa katika neema au adhabu mpaka pale zitaporejea kwenye viwiliwili vyake. Haya yamesemwa wazi wazi na dalili.”

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Muhammad al-Hanbaliy al-Manbajiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Tasliyatu Ahl-il-Maswaa-ib, uk. 218-219
  • Imechapishwa: 14/12/2016