Swali 100: Baadhi ya watu wanawaweka baadhi ya maimamu katika Bid´ah kama vile Ibn Hajar, an-Nawawiy, Ibn Hazm, ash-Shawkaaniy na al-Bayhaqiy. Je, ni sahihi?

Jibu: Maimamu hawa wana ubora, elimu nyingi, kuwanufaisha watu, kujitahidi kuihifadhi na kuieneza Sunnah na tungo kubwa ambazo zinafunika yale makosa walionayo. Allaah awarehemu. Tunamshauri mwanafunzi asijishughulishe na mambo haya, kwa sababu yanamkosesha mtu elimu. Ambaye anafuatilia mambo haya kwa maimamu basi atanyimwa kujifunza elimu. Matokeo yake atashughulishwa na fitina na magomvi na watu. Tunawanasihi wote kutafuta elimu na kujishughulisha nayo badala ya mambo yasiyokuwa na faida.

an-Nawawiy, Ibn Hazm, Ibn Hajar, ash-Shawkaaniy na al-Bayhaqiy ni maimamu wakubwa. Wanazuoni wanawaamini. Wanazo tungo kubwa na marejeo ya Kiislamu ambayo mpaka hii leo waislamu wanazirejelea. Matendo yao yanafunika makosa yao. Allaah awarehemu. Lakini sasa, wewe masikini, una kipi ulichokuja nacho? Wewe ambaye unatafuta na kuwapekua Ibn Hajar, Ibn Hazm na wengineo waliyotajwa katika swali – umewanufaisha waislamu kwa lipi? Ni kipi ulichokusanya katika elimu? Unayajua yale anayoyajua Ibn Hajar na an-Nawawiy? Je, umewafanyia waislamu yale aliyowafanyia Ibn Hazm na al-Bayhaqiy? Allaah ametakasika kutokana na mapungufu! Allaah amrehemu mtu ambaye anatambua kiwango chake. Ni chache elimu yako – ukafanya ujasiri. Uchaji wako ni mchache – ukazungumza.

  • Muhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Ajwibah al-Mufiydah ´an As-ilat-il-Manaahij al-Jadiydah, uk. 234-237
  • Imechapishwa: 12/08/2024
  • Mkusanyaji: Shaykh Jamaal bin Furahyaan al-Haarithiy