100. Roho imeumbwa au ni ya tangu hapo kale?

Je, roho zimeumbwa baada ya kutokuwepo kwake au zilikutwa tangu hapo kale? ´Allaamah Ibn-ul-Qayyim amesema:

“Katika masuala haya wameteleza wanachuoni wengi na kundi kubwa limepotea ilihali Allaah amewaongoza katika haki ya wazi wafuasi wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Mitume wote (Swalla Allaahu ´alayhim wa sallam) wameafikiana juu ya kwamba roho zimeumbwa, zimeundwa na ni zenye kuendeshwa. Hili ni jambo linalojulikana fika katika Uislamu na kwamba viumbe wote wameumbwa, viwiliwili vitafufuliwa na kwamba Allaah peke yake ndiye Muumbaji na vyengine vyote vimeumbwa. Upotevu ulitokea baadaye. Kuna baadhi wenye uelewa mfinyu juu ya Qur-aan na Sunnah ambao wamedai kuwa roho ni ya tangu kale na kwamba haikuumbwa kwa sababu eti ni katika amri ya Allaah na kwamba amri ya Allaah haikuumbwa na kwamba Ameinasibisha roho Kwake kama alivyojinasibishia elimu Yake, uhai Wake na uwezo Wake. Kuna wengine waliolinyamazia hilo na hawakusema kuwa imeumbwa wala kwamba ni ya tangu hapo kale.”

Wakati Ibn Mandah alipoulizwa kama roho zimeumbwa au hazikuumbwa alijibu:

“Roho zote zimeumbwa. Haya ndio maoni ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah. Dalili yao ni maneno ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Roho ni wanajeshi walioshikana. Wale ambao wataafikiana watakuwa pamoja.”

Wanajeshi walioshikana hawawi vyengine isipokuwa wameumbwa.

Baadhi ya wengine wamesema kuwa roho ni katika amri ya Allaah na kwamba Allaah amewaficha viumbe uhalisia wa roho. Dalili yao ni:

وَيَسْأَلُونَكَ عَنِ الرُّوحِ ۖ قُلِ الرُّوحُ مِنْ أَمْرِ رَبِّي

“Wanakuuliza kuhusu roho. Sema: “Roho ni katika amri ya Mola wangu.” 17:85

Wengine wakasema kuwa roho ni nuru na uhai wa Allaah. Dalili yao ni maneno ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Allaah ameumba uumbaji Wake katika giza na akatupa nuru Yake juu yake.””

Muhammad bin Naswr al-Marwaziy amesema:

“Kundi la mazanadiki na Raafidhwah wameifasiri roho ya Aadam kama walivyofasiri manaswara roho ya ´Iysaa na wengine waliosema kuwa roho imeachana na dhati ya Allaah na imekita kwa muumini. Kundi la mazanadiki na Raafidhwah wamesema: “Roho ya Aadam haikuumbwa.” Maoni haya wamefasiri maneno ya Allaah (Ta´ala):

فَإِذَا سَوَّيْتُهُ وَنَفَخْتُ فِيهِ مِن رُّوحِي فَقَعُوا لَهُ سَاجِدِينَ

“Nitakapomsawazisha na nikampuliza kitu katika roho Yangu, basi muangukieni kumsujudia.” 15:29

ثُمَّ سَوَّاهُ وَنَفَخَ فِيهِ مِن رُّوحِهِ

“Kisha Akamsawazisha na akapuliza humo kitu katika roho Yake.” 32:09

Baada ya maneno marefu akasema:

“Hakuna tofauti kati ya waislamu juu ya kwamba roho zilizo kwa Aadam, wanawe na wengine wote zimeumbwa na Allaah. Allaah ameziumba, akazileta, akaziunda na kuzitenegeneza.”

Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah amesema:

“Roho ya mwanaadamu imeumbwa na kuundwa kwa mujibu wa Salaf, maimamu na Ahl-us-Sunnah waliobaki. Wanachuoni wengi wa waislamu akiwemo Muhammad bin Naswr al-Marwaziy na Ibn Qutaybah wamesimulia maafikiano ya wanachuoni juu ya kwamba roho imeumbwa.”

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Muhammad al-Hanbaliy al-Manbajiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Tasliyatu Ahl-il-Maswaa-ib, uk. 217-218
  • Imechapishwa: 11/12/2016