Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Dalili ya khofu ni Kauli Yake (Ta´ala):

فَلَا تَخَافُوهُمْ وَخَافُونِ إِن كُنتُم مُّؤْمِنِينَ

“Basi msiwakhofu – na nikhofuni Mimi, mkiwa ni waumini.” (Aal ´Imraan 03 : 175)

MAELEZO

Pindi mwandishi (Rahimahu Allaah) alipotaja aina mbalimbali za ´ibaadah akataja vilevile khofu. Kuna aina tatu za khofu:

1- Khofu yenye kufichikana. Khofu hii anatekelezewa Allaah pekee kwa kuwa Yeye ndiye muweza wa kila jambo. Yeye ndiye ambaye anakhofiwa na kuogopwa. Allaah (Ta´ala) amesema:

فَلَا تَخَافُوهُمْ وَخَافُونِ إِن كُنتُم مُّؤْمِنِينَ

“Basi msiwakhofu – na nikhofuni Mimi, mkiwa ni waumini.” (03:175)

وَلَمْ يَخْشَ إِلَّا اللَّـهَ

“Hawamkhofu mwingine isipokuwa Allaah.” (09:18)

فَلَا تَخْشَوُا النَّاسَ وَاخْشَوْنِ

“Msiwaogope watu niogopeni Mimi.” (05:44)

Lililo la wajibu ni kumkhofu na kumuogopa Allaah. Kwa kuwa Yeye ndiye mwenye kuzigeuza na kuzipindua nyoyo na ndiye muweza juu ya kila jambo. Yeye ndiye anayenufaisha na kudhuru, kutoa na kuzuia. Ni wajibu kumuogopa Yeye pekee. Katika mambo yote asiogopwe mwengine isipokuwa Allaah pekee. Aina hii ya khofu anatakiwa atekelezewe Allaah pekee. Inahusiana na mtu kuogopa uwezo maalum na uliyofichikana, na sio kwa kitu chenye kuhisiwa. Kwa ajili hiyo baadhi ya waabudu makaburi wanaamini kuwa kuna watu wenye uwezo wa kuuendesha ulimwengu pamoja na Allaah (Jalla wa ´Alaa). Hali kadhalika wanaonelea juu ya masanamu, majini na vyenginevyo. Hii ni shirki kubwa. Wanaitakidi kuwa wana uwezo wa kutoa na kuzuia, kupotoa na kufisha kwa njia isiyokuwa ya kihisia.

2- Khofu juu ya vitu vyenye kuhisiwa. Aina ya khofu hii imetajwa na Allaah (Ta´ala) katika kisa kuhusu vita vya Uhud. Pindi Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipopata khabari kuwa washirikina wako njiani wanawarejelea, ndipo Allaah akateremsha:

إِنَّمَا ذَٰلِكُمُ الشَّيْطَانُ يُخَوِّفُ أَوْلِيَاءَهُ فَلَا تَخَافُوهُمْ وَخَافُونِ إِن كُنتُم مُّؤْمِنِينَ

“Hakika huyo ni shaytwaan anawakhofisha wapenzi wake. Basi msiwakhofu – na nikhofuni Mimi, mkiwa ni waumini.” (03:175)

Shaytwaan anawakhofisha watu kwa marafiki zake. Anawafanya waonekane wakubwa ili waogopwe. Lakini Allaah anasema:

فَلَا تَخَافُوهُمْ

“Basi msiwakhofu.”

Bali nitegemeeni, fanyeni maandalizi na msiwajali. Allaah (Ta´ala) amesema:

وَأَعِدُّوا لَهُم مَّا اسْتَطَعْتُم مِّن قُوَّةٍ وَمِن رِّبَاطِ الْخَيْلِ تُرْهِبُونَ بِهِ عَدُوَّ اللَّـهِ وَعَدُوَّكُمْ وَآخَرِينَ مِن دُونِهِمْ لَا تَعْلَمُونَهُمُ اللَّـهُ يَعْلَمُهُمْ

“Waandalieni nguvu zozote mziwezazo na farasi waliofungwa tayari muwaogopeshe kwayo maadui wa Allaah na maadui zenu na wengineo wasiokuwa wao, hamuwajui lakini Allaah anawajua.” (08:60)

Khofu kama hii yenye kuhisiwa haina neno. Khofu yenye kufichikana ndio imekatazwa. Khofu yenye kuhisiwa ni kwa mfano mtu kuogopa majambazi, wezi au maadui. Katika hali hii mtu anatakiwa ajiandae kwa silaha zinazohitajika. Kwa ajili hiyo Allaah (Ta´ala) amesema:

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا خُذُوا حِذْرَكُمْ فَانفِرُوا ثُبَاتٍ أَوِ انفِرُوا جَمِيعًا

“Enyi mlioamini! Chukueni tahadhari na tokeni kwa vikosi vikosi au tokeni kwa pamoja.” (04:71)

Allaah (Subhaanah) amesema kuhusu Muusa (´alayhis-Salaam) pindi alipokimbia kutoka Misri akimuogopa Fir´awn na watu wake:

فَخَرَجَ مِنْهَا خَائِفًا يَتَرَقَّبُ ۖ قَالَ رَبِّ نَجِّنِي مِنَ الْقَوْمِ الظَّالِمِينَ

“Basi akatoka humo akiwa na khofu anaangaza kwa tahadhari. Akasema: “Mola wangu! Niokoe na watu madhalimu.”” (28:21)

Kuogopa vitu vyenye kuhisiwa ni kama tulivyosema haina neno. Lakini hata hivyo haifai kumuogopa adui kiasi cha kwamba mtu akashindwa kutoka kwenda katika mapambano na kuinusuru haki. Badala yake khofu hii imfanye mtu kujiandaa kwa ajili ya adui na kutahadhari nae.

3- Khofu ya kimaumbile. Ni maumbile ya mtu kuwa na khofu kama hii. Haina neno. Ni kama mfano mtu kuogopa nge, nyoka na wadudu wakali ambapo anajiweka mbali nao na anawaua. Mtu anatakiwa kujitenga mbali na sehemu kama hizo ili wasimdhuru. Hili ni jambo lisiloepukwa. Allaah amewaumba watu kwa maumbile ya kuogopa vyenye kudhuru ili waviepuke. Mtu anaogopa baridi na hivyo anavaa mavazi mazito. Anaogopa njaa na hivyo anakula. Anaogopa kiu na hivyo anakunywa maji. Haya ni mambo ya kimaumbile na yasiyokuwa na neno.

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 33-34
  • Imechapishwa: 11/12/2016