Ndugu! Mwezi wa Ramadhaan umekaribia kumalizika na ni wenye kukutoleeni ushuhuda au ni wenye kutoa ushahuda dhidi yenu kutokana na yale matendo mliyofanya ndani yake. Yule ambaye ameuaga kwa matendo mema, basi amshukuru Allaah kwa hilo na apate bishara ya malipo mazuri, kwani hakika Allaah hapotezi ujira wa wafanyao mema. Na yule ambaye ameuaga kwa matendo maovu, bas atubie kwa Allaah tawbah ya kweli, kwani Allaah ni mwenye kumsamehe mwenye kutubia.

Katika kumalizia mwezi wenu Allaah amekuwekeeni ´ibaadah mbalimbali zinazokuwekeni karibu zaidi na Allaah na zinaifanya imani yenu kuwa na nguvu zaidi na mema katika madaftari ya matendo yenu. Allaah akaweka katika Shari´ah Zakaat-ul-Fitwr, ambayo tumekwishaizungumza kwa upambanuzi. Aidha amekuwekeeni Shari´ah ya kuleta Takbiyr kuanzia pale jua linapozama usiku wa kuamkia ´iyd mpaka wakati wa kwenda kuswali ´iyd. Amesema (Ta´ala):

وَلِتُكْمِلُوا الْعِدَّةَ وَلِتُكَبِّرُوا اللَّـهَ عَلَىٰ مَا هَدَاكُمْ وَلَعَلَّكُمْ تَشْكُرُونَ

”… ili mkamilishe idadi na ili mumkabiri Allaah kwa kuwa amekuongozeni na mpate kushukuru.”[1]

Namna yake ni kusema:

الله أكبر الله أكبر لا إِله إِلاَّ الله والله أكبر الله أكبر ولله الحمد

“Allaah ni mkubwa, Allaah ni mkubwa, hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah, na Allaah ni mkubwa, Allaah ni mkubwa, himdi zote njema anastahiki Yeye.”

Inapendeza wanaume waiseme kwa sauti ya juu masokoni, majumba hali ya kutangaza kumtukuza Allaah na wadhihirishe kumwabudu na kumshukuru. Wanawake wao wataisema kimyakimya kwa sababu wao wameamrishwa kufanya kimyakimya sauti zao.

Ni uzuri uliyoje wa hali za watu pindi wanapomkabiri Allaah hali ya kumtukuza kila mahali wakati wanapomaliza mwezi wa swawm yao. Wanajaza upeo wa macho Takbiyr, Tahmiyd na Tahliyl hali ya kuwa ni wenye kutaraji rehema za Allaah na kuogopa adhabu Zake.

[1] 02:185

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majaalis Shahr Ramadhwaan, uk. 223-224
  • Imechapishwa: 27/03/2024