Mitume (Swalla Allaahu ´alayhim wa sallam) ndio watu wakweli zaidi. Wamesimamisha dalili na miujiza juu ya ukweli wao. Wametukhabarisha juu ya hayo na kwamba haya ni uumbaji wa Allaah, kwamba Yeye ni Mola na Muumba wetu, kwamba Yeye ni Mwingi wa huruma, Mwenye kurehemu, kwamba Yeye ni as-Salaam, kwamba Yeye ni al-Qudduus na majina mengineyo mazuri mno (Subhaanahu wa Ta´ala). Ni kama ambavo Yeye (´Azza wa Jall) ameeleza ndani ya Kitabu Chake kitukufu ya kwamba ni Mwingi wa hekima, Mjuzi wa kila kitu na Muweza wa kila kitu (Jalla wa ´Alaa).

Katika haya kuna majibu barabara kwa walinganizi wa kikomunisti, watu wanaokanusha uwepo wa Mungu, watu wenye mrengo wa kijamaa na wengineo wanaopinga uwepo wa Allaah. Je, viumbe hivi vinajiumba na kujikuza vyenyewe? Je, haya yanasemwa na mwenye akili? Bali endapo utamwambia mtu eti kikombe cha maji kimejiumba chenyewe atakuona kuwa ni mwendawazimu. Vivyo hivyo kikombe cha chai, kikombe cha kahawa, kijiko na bakora. Vyote hivi anatambulika aliyevitengeneza. Tusemeje kuhusu ulimwengu huu mkubwa ambao umeumbwa na Muumba baada ya kutokuwepo kwake na akaweka ndani alama na manufaa yasiyohesabika. Yeye ndiye Aliyevianzilisha – Ametakasika (Ta´ala) juu ya yale wanayosema kutakasika kukubwa.

Isitoshe Muumba huyu amebainisha majina yanayolingana na dhati Yake na Mitume Yake wakabainisha sifa na majina Yake. Aidha wakatambuza na kuelekeza kwayo. Dalili zimesimama kwa mujibu wa ukweli wao. Ambaye yuko katika kilele chao ni Mtume wetu Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Yeye ndiye Mtume mkweli zaidi na mbora wao. Allaah amemtumiliza kwa Kitabu Chake kitukufu na ujumbe wake ulioenea ambao umeweka wazi kila kitu.

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ahamiyyat-ul-´Ilm https://binbaz.org.sa/discussions/33/اهمية-العلم-في-محاربة-الافكار-الهدامة
  • Imechapishwa: 12/04/2022