10. Swalah ya mwanamke inapoonekana miguu au nywele zake

Swali 10: Wanawake wengi wanachukulia wepesi katika jambo la swalah ambapo inaonekana mikono yao au sehemu yake na vivyo hivyo nyayo zao na pengine baadhi ya miundi yao. Je, swalah yake ni sahihi katika kipindi hicho?

Jibu: Ni lazima kwa mwanamke muungwana na ambaye ´ibaadah ni yenye kumuwajibikia kufunika mwili wake mzima ndani ya swalah isipokuwa uso na viganja vya mikono. Mwili wake mzima ni uchi. Akiswali na akaacha wazi kitu katika uchi wake, kama vile muundi, nyayo, kichwa chote au sehemu yake, basi swalah yake haisihi. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Allaah haikubali swalah ya mwenye hedhi isipokuwa kwa Khimaar.”

Ameipokea Ahmad na watunzi wa Sunan isipokuwa an-Nasaa´iy kwa cheni ya wapokezi Swahiyh.

Makusudio ya mwenye hedhi ni yule mwanamke aliyebaleghe. Vilevile amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Mwanamke ni uchi.”

Abu Daawuud amepokea kupitia kwa Umm Salamah (Radhiya Allaahu ´anhaa) ambaye ameeleza kuwa alimuuliza Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuhusu mwanamke anayeswali ndani ya shuka ya juu na ushungi pasi na shuka ya chini ambapo akasema:

“Ikiwa shuka yake ya juu ni pana basi afunike mgongo na miguu yake.”

Haafidhw Ibn Hajar (Rahimahu Allaah) amesema katika “Buluugh-ul-Maraam”:

“Maimamu wameisahihisha kuishilia kwa Umm Salamah (Radhiya Allaahu ´anhaa).”

Ikiwa kuna mbele yake wanamme wa kando naye basi analazimika pia kufunika uso na viganja vyake vya mikono.

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fataawaa Muhimmah, uk. 10-11
  • Imechapishwa: 11/08/2022