Imepokelewa katika Hadiyth nyingine ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ameeleza mwezi huu ya kwamba ni mwezi wa subira na akasema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Funga ya mwezi wa subira na funga ya masiku matatu kila mwezi ni kama kufunga mwaka mzima.”[1]

Ameueleza kuwa ni mwezi wa subira. Maana yake ni kwamba ndani ya mwezi huu mtukufu muislamu anayo fursa kubwa ya kuifua na kuizoweza nafsi yake kuwa na subira kwa aina zake zote:

1 – Subira juu ya kumtii Allaah.

2 – Subira ya kuacha kumuasi Allaah.

3 – Subira juu ya makadirio ya Allaah (Tabaarak wa Ta´ala).

Huu ni msimu wa subira.

Allaah atawalipa wenye kusubiri malipo yao bila ya hesabu. Mwezi wa Ramadhaan ni kipindi kikubwa cha subira. Muislamu, kuanzia siku ya kwanza katika masiku ya mwezi huu mtukufu, aizoweze nafsi yake kuwa na subira. Subira juu ya ´ibaadah, subira ya kumtii Allaah, subira ya kumtaja Allaah, subira ya kusoma Qur-aan, subira ya kuswali, subira ya kufunga na mengineyo ambayo Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) ameamrisha kumwabudu nayo.

Vilevile aizoweze nafsi yake kuwa na subira ya kuacha kumuasi Allaah. Hivyo ayaache yale mambo aliyoyazowea kukiwemo vyakula, vinywaji na mengineyo katika mchana wa Ramadhaan. Asubiri juu ya hayo kwa ajili ya kumtii Allaah (Tabaarak wa Ta´ala).

Aidha aipe mazoezi nafsi yake ya kusubiri juu ya makadirio ya Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) yanayoumiza. Kuacha chakula na kinywaji nafsi inatamani mambo hayo. Vivyo hivyo kuizuia nafsi kutokamana na vile vitu alivyoruhusu Allaah katika yale mambo ya matamanio na ya burudani kukiwemo jimaa na vile vitangulizi vyake ni jambo linalomsaidia mtu kuihakikisha subira hii.

Matokeo yake muislamu anaishi ndani ya mwezi huu hali ya kuwa ni mwenye subira mpaka hatimaye anatoka hali ya kuwa amepata mafunzo makubwa kuhusu subira na amezowea milango mingi ya kheri. Hivyo mwezi unakuwa umemrudilia mtu – na si katika mwezi mmoja pekee – bali baraka na kheri za mwezi zimemrudilia na kuyabadilisha maisha na umri wake wote. Kwa sababu ameipa mazoezi nafsi yake kuwa na subira na ameishi na subira katika msimu mtukufu. Ikiwa muislamu hapambiki kuwa na subira katika msimu wake mkubwa, basi ni lini atakuwa na subira?

Kwa ajili hiyo miongoni mwa mambo muhimu ambayo muislamu anapaswa kuyatilia umuhimu ni yeye kujizoeza ndani ya mwezi huu mtukufu kuwa na subira kwa aina zake zote:

1 – Subira juu ya kumtii Allaah.

2 – Subira ya kuacha kumuasi Allaah.

3 – Subira juu ya makadirio ya Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) yanayoumiza.

[1] Ahmad (7567) na an-Nasaa´iy (2408) kupitiak wa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh). Ni Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy.

  • Mhusika: Shaykh ´Abdur-Razzaaq bin ´Abdil-Muhsin al-´Abbaad
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Wa jaa´ Shahru Ramadhwaan, uk. 12-15
  • Imechapishwa: 12/04/2022