10. Mke mwema anamuhudumikia mume wake

4 – Mwenye kumhudumikia mume wake. Mwanzo wa huduma hiyo ni katika nyumba yake na yaliyofungamana na hayo katika kuwalea watoto, kuandaa chakula, kutandika na mfano wa hayo. Huswayn bin Muhswan ameeleza: “Shangazi yangu amenihadithia akisema: “Nilienda kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) nikiwa ni mwenye kuhitajia baadhi ya haja ambapo akasema: “Je, wewe una mume?” Nikajibu: “Ndio.” Akasema: “Uko vipi kwake?” Nikajibu: “Sina upungufu katika kumtii na kumhudumia isipokuwa yale yanayonishinda.” Akasema: “Angalia vizuri uhusiano wako kwake! Kwani yeye ndiye [ufunguo wako] wa Pepo na wa Moto.”[1]

Huu hapa mfano wa huduma ya Asmaaa´ bint Abiy Bakr (Radhiya Allaahu ´anhumaa). Amesema:

”az-Zubayr alinioa na hakuwa akimiliki kitu isipokuwa farasi. Nilikuwa nikimpa chakula na maji na nikishona ndoo yake kubwa na kutengeneza unga. Sikuwa mzuri wa kutengeneza wa kutengeneza mkate, hivyo nilikuwa na wasichana wa ki-Answaar wanaonifanyia na walikuwa wazuri na wanawake waaminifu. Nilikuwa nikibeba juu ya kichwa changu kokwa za tende kutoka katika ardhi ya az-Zubayr ambayo alipewa na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) iliokuwa theluthi mbili za Farsakh kutokea nyumbani kwangu. Siku moja nilikuwa na kokwa za tende kichwani mwangu ambapo ghafla nikakutana na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akiwa pamoja na baadhi ya Maswahabah zake. Akaniita na kusema ”Ikh, Ikh”[2] ili anibebe nyuma yake. Nikaona haya na nikakumbuka wivu wako. Ndipo akasema: ”Naapa kwa Allaah kwamba kubeba kokwa za tende kulikuwa ni kukubwa zaidi kwangu kuliko kupanda pamoja naye.”Baada ya hapo Abu Bakr akanitumia mfanya kazi wa kike kuja kumshughulikia huyo farasi na ilikuwa ni kana kwamba ameniacha huru.”[3]

Wanazuoni wamekinzana kuhusu hukumu ya mwanamke kumhudumikia mume wake. Shaykh-ul-Islaam amesema:

“Wanazuoni wametofautiana kama mke analazimika kumhudumikia katika mfano wa kutandika nyumba, kumtayarishia chakula na kinywaji, mkate, kusaga unga, kuwapa chakula watumwa wake, wanyama wake na mfano wa mambo kama hayo? Wako waliosema kuwa si lazima kumhudumikia. Maoni haya ni dhaifu. Ni kama udhaifu wa maoni yanayosema kuwa si lazima kwa mume kuishi kwa wema na kumwingilia. Maoni mengine – na ndio ya sawa – ni kwamba ni lazima kumhudumikia. Mume ndiye bwana wake kwa mujibu wa Kitabu cha Allaah na mwanamke ni kama mfano wa mateka kwa mume kwa mujibu wa Sunnah ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam)[4]. Ni lazima kwa mtumwa na mjakazi kumhudumikia bwana wake. Jengine hilo ndilo linalotambulika.”

Amesema tena:

“Hakika maneno Yake Allaah (Ta´ala):

فَالصَّالِحَاتُ قَانِتَاتٌ حَافِظَاتٌ لِّلْغَيْبِ بِمَا حَفِظَ اللَّـهُ

“Basi wanawake wema ni wale watiifu wenye kujihifadhi katika hali ya kutokuweko waume zao kwa kuwa Allaah ameamrisha wajihifadhi.”[5]

yanapelekea ulazima wa kumtii mume moja kwa moja kukiwemo kumhudumikia, kusafiri naye, kummakinisha mume na mengine yote kama ambavo inalazimika kuwatii wazazi wawili. Kwani hakika kila utiifu uliokuwa kwa wazazi wawili unahama na kwenda kwa mume.”[6]

[1] al-Haakim (02/189) na wengineo. al-Haakim ameisahihisha na adh-Dhahabiy akaafikiana naye na al-Albaaniy akakubaliana naye katika ”Aadaab-iz-Zifaaf”, uk. 285.

[2] Ibn Hajar amesema:

”Ni maneno anayoambiwa ngamia ili apige magoti.” (Fath-ul-Baariy (9/389))

[3] al-Bukhaariy (09/319), Muslim (2182) na wengineo.

[4] Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema katika Khutbah ya kuaga:

”Zindukeni! Nakuusieni kuwatendea wema wanawake. Kwani hakika wao ni mateka kwenu.”

Ameipokea kwa tamko hili at-Tirmidhiy (1163) ambaye amesema kuwa ni nzuri na Swahiyh, Ibn Maajah (1851). al-Albaaniy ameipa nguvu katika ”al-Irwaa´-ul-Ghaliyl” (07/52).

[5] 04:24

[6] Majmuu´-ul-Fataawaa (34/90) kwa kifupi.

  • Mhusika: Shaykh Muhammad Shuwmaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Swifaat-uz-Zawjah as-Swaalihah, uk. 24-28
  • Imechapishwa: 26/09/2022