09. Watu wanaochwa huru na Moto kila usiku wa Ramadhaan

Maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Kuna watu Allaah huwaacha huru na Moto na hilo linakuwa katika kila usiku.”3

Bi maana Allaah (Jalla wa ´Alaa) katika kila usiku wa mwezi huu mtukufu huwaacha huru baadhi ya watu kutoka Motoni. Muislamu anatamani apate kufuzu huku kukubwa; kuachwa huru na Moto – Allaah atulinde sote kutokamana na Moto.

Wakati fulani katika baadhi ya maeneo hutangazwa mashindano na zawadi. Kila siku kunatengwa zawadi aidha ya SAR 1000 au zaidi au chini ya hapo. Utawaona watu wanaharakia kwenda maeneo hayo kwelikweli na wanarundikana. Kila mmoja anafika, anajitolea na anajipinda kwelikweli ili aweze kupata SAR 1000 au zaidi au chini ya hapo na awe miongoni mwa wenye kufuzu. Lakini inapokuja katika suala la kufuzu huko Aakhirah na thawabu siku ya Qiyaamah shauku inakuwa ndogo, hamu inadhoofika na yanafupika matakwa ya watu kwa kitu kama hiki kitukufu. Vinginevyo kinachompasa muislamu wakati anaposikia maneno yake Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Kuna watu Allaah huwaacha huru.”

aingiwe na shauku ya jambo hilo na apupie awe miongoni mwa watu hawa. Anatakiwa ajipinde, kujitahidi, amwombe Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) amwache huru kutokamana na Moto na amwelekee Allaah (Jalla wa ´Alaa) ili aweze kupata ahadi hii tukufu na thawabu hizi kuu.

[3] at-Tirmidhiy (682) na Ibn Maajah (1642). Ni Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy.

  • Mhusika: Shaykh ´Abdur-Razzaaq bin ´Abdil-Muhsin al-´Abbaad
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Wa jaa´ Shahru Ramadhwaan, uk. 11-12