08. Kama hukujirudi katika Ramadhaan utajirudi lini?

at-Tirmidhiy amepokea katika “a-Sunan” yake kupitika kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye ameeleza kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akisema:

“Usiku wa kwanza wa Ramadhaan mashaytwaan na wale majini waovu hutiwa pingu, milango ya Moto hufungwa ambapo hakufunguliwi mlango wowote na milango ya Pepo hufunguliwa ambapo hakufungwi mlango wowote. Ananadi Mwenye kunadi: “Ee mwenye kutaka kheri! Njoo! Ee mwenye kutaka shari! Koma!” Kuna watu Allaah huwaacha huru na Moto na hilo linakuwa katika kila usiku.”2

Zingatia maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Ananadi Mwenye kunadi: “Ee mwenye kutaka kheri! Njoo!“

Bi maana umekujia msimu wenye kheri na msimu wa kumtii Allaah. Hivyo ukimbilie kwa haraka na upupie pupa kubwa. Tahadhari tena tahadhari kujipotezea fursa hii kubwa. Huu ni msimu wa kupata faida ya kheri na biashara yake ni yenye faida. Ukishaondoka basi haurudi. Maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Ee mwenye kutaka shari! Koma!”

Bi maana haistahiki kwa wewe mwenye kutaka shari au nafsi yake inaichangamkia shari kuipa nafasi ikaendelea katika shari yake, kupindukia mipaka katika uasi wake na ikaendelea katika upotofu wake katika kipindi hichi kitakatifu na kilichobarikiwa.

Ambaye hatoichangamsha nafsi yake kumwelekea Allaah (Tabaarak wa Ta´ala), kutubu na kujutia wakati kunapofika kipindi kama hichi kitukufu, basi lini nafsi yake itapata uchangamfu? Watu wengi wameghilibiwa na shughuli na mambo ya pumbao na vitu hivyo vimekuwa ni kizuizi kikubwa kutokamana na wao kutubu na kurejea kwa Allaah. Akipambazukiwa na asubuhi na akiingiliwa na jioni yuko katika anasa, israfu, ubadhirifu, michezo, kukesha, kulala, kuzembea, dhuluma na maovu. Kwa hivyo mwezi wa Ramadhaan ni fursa kwa watu kama hawa wapumbaaji kwa ajili ya kutubu tawbah ya kweli na kuelekea kwa Allaah. Ikiwa nafsi yako haikutikisika katika kipindi kama hiki kitukufu ikakufanya uweze kutubia, basi ni lini itatikisika? Ikiwa mja hakuelekea kwa Allaah katika mwezi huu uliyobarikiwa, basi ni lini atamwelekea?

  • Mhusika: Shaykh ´Abdur-Razzaaq bin ´Abdil-Muhsin al-´Abbaad
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Wa jaa´ Shahru Ramadhwaan, uk. 10-11
  • Imechapishwa: 08/04/2022