37 – Abu Mu´aawiyah ametuhadithia: kutoka kwa ´Aaswim Abu ´Uthmaan, kutoka kwa Salmaan aliyesema:

”Ataambiwa, bi maana Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam): ”Shufai utakubaliwa, omba utaitikiwa. Omba du´aa utakubaliwa.” Atanyanyua kichwa chake na kusema: ”Ee Mola, ummah wangu!” Atasema hivo mara mbili au mara tatu. Atamfanyia uombezi kila ambaye moyoni mwake kulikuwa na imani sawa na uzito wa punje ya ngano, au sawa na uzito wa punje ya shayiri, au sawa na uzito wa punje ya hardali. Hicho ndio cheo chenye kusifiwa.”[1]

38 – Yaziyd bin Haaruun ametuhadithia: Muhammad bin ´Amr ametueleza, kutoka kwa Abu Salamah, kutoka kwa Abu Hurayrah ambaye amesimulia kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Hazini mwenye kuzini pale anapozini hali ya kuwa ni muumini, hanywi pombe mwenye kunywa pombe pale anapokunywa hali ya kuwa ni muumini na wala hapori kitu, jambo linalofanya watu kumuinulia macho, hali ya kuwa ni muumini.”[2]

39 – Yaziyd bin Haaruun ametuhadithia: Muhammad bin Ishaaq ametueleza, kutoka kwa Yahyaa bin ´Abbaad bin ´Abdillaah bin az-Zubayr, kutoka kwa baba yake, kutoka kwa ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) ambaye ameeleza kuwa amemsikia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akisema:

“Hazini mwenye kuzini pale anapozini hali ya kuwa ni muumini, haibi pale anapoiba hali ya kuwa ni muumini na wala hanywi – yaani pombe – pale anapokunywa hali ya kuwa ni muumini. Jihadharini, jihadharini!”[3]

40 – Ibn ´Ulayyah ametuhadithia, kutoka kwa al-Layth, kutoka kwa Mudrik, kutoka kwa Ibn Abiy Awfaa ambaye ameeleza kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Hazini mwenye kuzini pale anapozini hali ya kuwa ni muumini, haibi mwenye kuiba pale anapoiba hali ya kuwa ni muumini, hanywi pombe pale anapokunywa hali ya kuwa ni muumini na wala hapori kitu chenye thamani, jambo linalofanya watu kumuinulia vichwa vyao, hali ya kuwa ni muumini.”[4]

41 – al-Hasan bin Muusa ametuhadithia: Shu´bah ametueleza, kutoka kwa Firaas, kutoka kwa Mudrik, kutoka kwa Ibn Abiy Awfaa ambaye amesimulia mfano wake kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

 42 – Muhammad bin Bishr ametuhadithia: Muhammad bin ´Amr ametueleza, kutoka kwa Abu Salamah, kutoka kwa Abu Hurayrah ambaye amesimulia kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Hayaa ni katika imani. Imani iko Peponi. Maneno machafu ni katika ukengeukaji, na ukengeukaji ni Motoni.”

43 – Husayn bin ´Aliy ametuhadithia, kutoka kwa Zaaidah, kutoka kwa Hishaam, kutoka kwa al-Hasan, kutoka kwa Jaabir bin ´Abdillaah ambaye amesema:

“Kulisemwa: “Ee Mtume wa Allaah, ni imani ipi bora?” Akasema: “Subira na uvumilivu.” Kukasemwa: “Ni waumini wepi wenye imani kamilifu zaidi?” Akasema: “Ni wale wenye tabia njema zaidi.”[5]

[1] Cheni ya wapokezi ni Swahiyh. Ni maneno ya Swahabah, lakini yenye hukumu moja kama maneno ya Mtume kwa sababu kitu kama hicho hakisemwi kutokana na vile mtu anavyoona.

[2] Hadiyth ni Swahiyh na cheni ya wapokezi wake ni nzuri. Ameipokea al-Bukhaariy, Muslim na wengineo kupitia njia nyingine kutoka kwa Abu Hurayrah.

[3] Hadiyth ni Swahiyh. Wapokezi wake ni waaminifu ingawa tu Ibn Ishaaq hakueleza amesikia kutoka kwa nani. al-Haythamiy amesema:

“Ameipokea Ahmad, al-Bazzaar sehemu yake na at-Twabaraaniy katika “al-Mu´jam al-Awsatw”. Wapokezi wake ni waaminifu. Isipokuwa tu Ibn Ishaaq ambaye ni mudallis. Wapokezi wa al-Bazzaar ni wapokezi wa Swahiyh.” (Majma´-uz-Zawaaid (1/100))

Muslim (1/55) ameipokea kupitia baadhi ya njia kutoka kwa Abu Hurayrah kwa ziada: “Jihadharini, jihadharini!”

[4] Cheni ya wapokezi wake ni nzuri kupitia Hadiyth inayofuata. Zote zinazungukia kwa Mudrik bin ´Ammaarah al-Qurashiy. Ibn Abiy Haatim ameitaja katika ”al-Jarh wat-Ta´diyl” (327) namna jopo wamepokea kutoka kwake. Ibn Hibbaan pia amemuweka katika ”ath-Thiqaat” (1/230).

[5] Hadiyth ni Swahiyh. Wapokezi wake ni waaminifu ingawa tu al-Hasan al-Baswriy hakueleza amesikia kutoka kwa nani. Hata hivyo inatiliwa nguvu na Hadiyth ya ´Amr bin ´Absah na ´Ubaadah bin as-Swaamit kwa Ahmad (4/385) pamoja na (5/318-319).

  • Mhusika: Imaam Abu Bakr ´Abdullaah bin Muhammad bin Abiy Shaybah al-Kuufiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Kitaab-ul-Iymaan, uk. 24-25
  • Imechapishwa: 09/07/2023
  • taaliki: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy