32 – Abu Mu´aawiyah ametuhadithia, kutoka kwa ash-Shaybaaniy, kutoka kwa Abu ´Ilaaqah, kutoka kwa ´Abdullaah bin Yaziyd al-Answaariy[1] ambaye amesema:

“Jiiteni kwa majina yenu ambayo Allaah amekuiteni nayo; Haniyfiyyah, Uislamu na imani.”

33 – ´Abdullaah bin Idriys ametuhadithia, kutoka kwa al-A´mash, kutoka kwa Shaqiyq, kutoka kwa Salamah bin Sabrah ambaye amesema:

“Mu´aadh bin Jabal alitutolea Khutbah akasema: “Nyinyi ni waumini na nyinyi ni watu wa Peponi!”

34 – ´Umar bin Ayyuub ametuhadithia, kutoka kwa Ja´far bin Burqaan ambaye amesema:

”´Umar bin ´Abdil-´Aziyz alituandikia: ”Hakika kishikilio cha dini na nguzo ya Uislamu ni kumwamini Allaah, kusimamisha swalah na kutoa zakaah. Hivyo basi, swalini swalah kwa wakati wake.”

35 – Muhammad bin Bishr ametuhadithia: Sa´iyd ametuhadithia, kutoka kwa Qataadah, kutoka kwa Anas aliyeeleza kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Atatoka Motoni yule ambaye alisema hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah na moyoni mwake kukawa kuna kheri sawa na uzito wa shayiri. Atatoka Motoni yule ambaye alisema hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah na moyoni mwake kukawa kuna kheri sawa na uzito wa nafaka ya ngano. Atatoka Motoni yule ambaye alisema hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah na moyoni mwake kukawa kuna kheri sawa na uzito wa punje ya mahindi.”[2]

36 – Yaziyd bin Haaruun ametuhadithia: Ibn Abiy Dhi´b ametuhadithia, kutoka kwa az-Zuhriy, kutoka kwa ´Aamir bin Sa´d, kutoka kwa baba yake ambaye amesema:

”Kikosi cha watu kilikuja kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kumuomba kitu ambapo akawapa – isipokuwa bwana mmoja katika wao. Sa´d akasema: ”Ee Mtume wa Allaah! Umewapa na ukamwacha fulani. Naapa kwa Allaah kwamba mimi namuona kuwa ni muumini.” Ndipo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: ”Au muislamu?”  Sa´d akasema: ”Naapa kwa Allaah kwamba mimi namuona kuwa ni muumini.” Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: ”Au muislamu?”  Sa´d akasema: ”Naapa kwa Allaah kwamba mimi namuona kuwa ni muumini.” Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: ”Au muislamu?”  Akasema hivo mara tatu na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema hivo mara tatu.”

[1] Cheni ya wapokezi ni Swahiyh. ´Abdullaah bin Yaziyd al-Answaariy al-Khatamiy al-Kuufiy alikuwa Swahabah mdogo.

[2] Cheni ya wapokezi ni kwa mujibu wa sharti za al-Bukhaariy na Muslim. Wote wawili wameipokea katika ”as-Swahiyh” zao kupitia kwa Sa´iyd bin Abiy ´Aruubah na Hishaam ad-Dastawaaiy, kutoka kwa Qataadah. Katika baadhi ya mapokezi Qataadah ametamka waziwazi amehadithia kutoka kwa nani.

  • Mhusika: Imaam Abu Bakr ´Abdullaah bin Muhammad bin Abiy Shaybah al-Kuufiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Kitaab-ul-Iymaan, uk. 23-24
  • Imechapishwa: 09/07/2023
  • taaliki: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy