Isitoshe Hadiyth zinazotambulika kuhusu kukamilika kwa imani, ikiwa ni pamoja na:

“Ni viumbe wepi ambao wana imani kamili zaidi?” Kukasemwa: “Malaika.” Halafu kukasemwa: “Sisi, ee Mtume wa Allaah?” Akasema: “Bali ni watu watakaokuja baada yenu.” Baada ya hapo akataja sifa zao[1].

“Miongoni mwa waumini wenye imani kamilifu zaidi ni wale katika nyinyi wenye imani bora zaidi.”[2]

“Mtu haamini imani kamilifu mpaka aache uwongo katika mzaha na katika migogoro ijapo atakuwa mkweli.”[3]

Vivyo hivyo kumepokelewa mfano wake au yanayofanana na hayo kutoka kwa ´Umar bin al-Khattwaab na Ibn ´Umar (Radhiya Allaahu ´anhumaa).

Miongoni mwa mambo yanayoliweka hilo wazi zaidi ni maneno yake Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuhusu Uombezi:

“Ndipo atoke Motoni ambaye moyoni mwake kulikuwa na imani sawa na punje ya shayiri, imani sawa na punje ya ngano au imani sawa na mduduchungu.”[4]

Maswahabah walikuwa wakisema:

“Ee Mtume wa Allaah! Hakika baadhi yetu tunahisi ndani ya nafsi zetu ambayo bora mtu aanguke kutoka juu mbinguni kuliko kuyazungumza.” Akasema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam): “Huo ni usafi wa imani.”[5]

Kadhalika imekuja katika Hadiyth ya ´Aliy (Radhiya Allaahu ´anh):

“Imani huanza moyoni kama doa jeupe. Kila ambavyo imani inaongezeka, ndivo huongezeka weupe huo.”[6]

Kuna mifano mingi kama hiyo ambayo kutarefuka kuitaja hapa na sasa. Yote yaliyotajwa yanabainisha kutofautiana kwa imani katika nyoyo na matendo. Yote, au angalau mengi katika hayo, yanafahamisha kuwa matendo mema ni katika imani. Vipi basi maandiko haya yatapingwa kwa kuyabatilisha na kuyakadhibisha?

[1] al-Hasan bin ´Arafah katika ”al-Juz’” (2/90)  yake kupitia kwa ´Amr bin Shu´ayb, kutoka kwa baba yake, kutoka kwa baba yake, kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Cheni ya wapokezi wake ni dhaifu. al-Haakim ameipokea kupitia kwa ´Umar na akaisahihisha na adh-Dhahabiy akaafikiana naye.

[2]  Swahiyh. Wanazuoni wengi wameisahihisha. Ibn Abiy Shaybah ameipokea kupitia kwa Abu Hurayrah, ´Aaishah na al-Hasan al-Baswriy, kwa hiyo rejea maelezo yangu huko.

[3] Ahmad (2/352-353) na (2/364) kupitia kwa Mak-huul, kutoka kwa Abu Hurayrah, kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Hata hivyo Mak-huul hakusikia kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh).

[4] al-Bukhaariy na Muslim kupitia kwa Anas (Radhiya Allaahu ´anh). Ibn Abiy Shaybah (35) pia ameipokea.

[5] Muslim (1/83) na Ahmad (2/397) kupitia kwa Abu Hurayrah.

[6] Maneno ni ya ´Aliy (Radhiya Allaahu ´anh). Ameipokea Ibn Abiy Shaybah (8). Cheni ya wapokezi wake imekatika, kama nilivyobainisha huko. 

  • Mhusika: Imaam Abu ´Ubayd al-Qaasim bin Sallaam
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Kitaab-ul-Iymaan, uk. 29-32
  • Imechapishwa: 21/06/2023
  • taaliki: Imaam Muhammad Naawswir-ud-Diyn al-Albaaniy