06 – Kuamini makadirio; ya kheri na ya shari.

Nguzo ya sita ni kuamini makadirio na kwamba Allaah ameyakadiria mambo kabla ya kuumba watu. Ni makadirio ambayo yametangulia. Muslim amepokea katika “as-Swahiyh” yake kupitia kwa ´Abdullaah bin ´Amr bin al-´Aasw (Radhiya Allaahu ´anhumaa) ambaye ameeleza kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Allaah ameyakadiria makadirio ya waja miaka elfu khamsini kabla kuumba mbingu na ardhi na ´Arshi Yake ilikuwa juu ya maji.”[1]

Amesema (Jalla wa ´Alaa):

إِنَّا كُلَّ شَيْءٍ خَلَقْنَاهُ بِقَدَرٍ

“Hakika sisi Tumekiumba kila kitu kwa makadirio.” (54:49)

مَا أَصَابَ مِن مُّصِيبَةٍ فِي الْأَرْضِ وَلَا فِي أَنفُسِكُمْ إِلَّا فِي كِتَابٍ مِّن قَبْلِ أَن نَّبْرَأَهَا ۚ إِنَّ ذَٰلِكَ عَلَى اللَّـهِ يَسِيرٌ لِّكَيْلَا تَأْسَوْا عَلَىٰ مَا فَاتَكُمْ وَلَا تَفْرَحُوا بِمَا آتَاكُمْ ۗ وَاللَّـهُ لَا يُحِبُّ كُلَّ مُخْتَالٍ فَخُورٍ

“Hakuna msiba wowote unaokusibuni katika ardhi au katika nafsi zenu isipokuwa umeandikwa katika Kitabu kabla Hatujauumba [huo msiba]. Hakika hayo kwa Allaah ni mepesi. Ili msisononeke juu ya yale yaliyokuondokeeni na wala msifurahie kwa yale Aliyokupeni; na Allaah Hapendi kila mwenye kujinata, anayejifakharisha.” (57:22-23)

Makadirio ni kitu kimetangulia, kisichoyumba na kiliandikwa. Amesema (Ta´ala):

أَلَمْ تَعْلَمْ أَنَّ اللَّـهَ يَعْلَمُ مَا فِي السَّمَاءِ وَالْأَرْضِ ۗ إِنَّ ذَٰلِكَ فِي كِتَابٍ ۚ إِنَّ ذَٰلِكَ عَلَى اللَّـهِ يَسِيرٌ

“Je, hujui kwamba Allaah anajua yale yote yaliyomo katika mbingu na ardhi? Hakika hayo yameandikwa katika Kitabu. Hakika hayo kwa Allaah ni mepesi.” (22:70)

Ahl-us-Sunnah wanaamini kuwa Allaah ameyakadiria mambo na kuyaandika miaka elfu khamsini kabla ya kuumba watu na kuumba vitu vyengine vyote. Wakati huo ´Arshi Yake ilikuwa juu ya maji.

Hizi ndio nguzo sita zinazohusiana na imani kwa mujibu wa Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah.

[1] Muslim (2653).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh al-´Aqiydah al-Waasitwiyyah, uk. 15
  • Imechapishwa: 16/10/2024