Suala hili la pili linahakikisha lile suala la kwanza, nalo ni kwamba unatakiwa kutambua kuwa Allaah haridhii kushirikishwa na yeyote katika ´ibaadah Yake. Kama jinsi Yeye ndiye Muumbaji na Mruzukaji anayehuisha na kufisha na ambaye amekuumba na kukupa neema, hakika Yeye (Subhaanah) haridhii kushirikishwa na kiumbe yeyote. Si Nabii aliyetumwa, Malaika aliyekaribu wala mwengine yeyote haifai kumuabudu. ´Ibaadah ni haki ya Allaah peke yake. Allaah (Ta´ala) amesema:

وَقَضَىٰ رَبُّكَ أَلَّا تَعْبُدُوا إِلَّا إِيَّاهُ

“Mola wako amehukumu kwamba, msimwabudu yeyote isipokuwa Yeye pekee.”” (17:23)

إِيَّاكَ نَعْبُدُ وَإِيَّاكَ نَسْتَعِينُ

“Wewe pekee ndiye tunakuabudu na Wewe pekee ndiye tunakuomba msaada.” (01:05)

Shirki ndio dhambi kubwa mno. Katika Aayah nyingi kumekuja maamrisho ya kumtakasia ´ibaadah Allaah peke yake na makatazo ya kumuabudu mwingine asiyekuwa Yeye. Hivyo unatakiwa kuoanisha kati ya mambo mawili; uamini kuwa Allaah ndiye Muumbaji na Mruzukaji anayehuisha na kufisha na unatakiwa vilevile kuamini kuwa Allaah ndiye mwenye kustahiki kuabudiwa kwa kichinjwa, swalah, swawm na mengineyo. Allaah (Subhaanah) amesema:

وَإِلَـٰهُكُمْ إِلَـٰهٌ وَاحِدٌ ۖ لَّا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ الرَّحْمَـٰنُ الرَّحِيمُ

“Muabudiwa wenu ni Mmoja pekee; hapana mungu wa haki isipokuwa Yeye, Mwingi wa Rahmah, Mwenye kurehemu.” (02:163)

وَأَنَّ الْمَسَاجِدَ لِلَّـهِ فَلَا تَدْعُوا مَعَ اللَّـهِ أَحَدًا

“Hakika sehemu zote za kuswalia ni kwa ajili ya Allaah; hvyo msiombe yeyote pamoja na Allaah.” (72:18)

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 15-16
  • Imechapishwa: 15/10/2016