09. Hapa ndipo utaanza na ile swalah ya sasa

Swali 09: Mtu akiwa amepitwa kwa mfano na Dhuhr ambapo akaikumbuka baada ya kukimiwa ´Aswr – je, ajiunge na mkusanyiko kwa nia ya ´Aswr au kwa nia ya Dhuhr au aswali Dhuhr kivyake kwanza kisha ndio aswali ´Aswr? Nini maana ya maneno ya wanazuoni:

“Akichelea kupitwa na ile swalah ya sasa basi unaanguka mpangilio wa swalah.”

Je, kuchelea kupitwa na swalah ya mkusanyiko kunadondosha ule mpangilio wa swalah?

Jibu: Kilichosuniwa kwa ambaye amelengwa katika swali aswali pamoja na mkusanyiko ilioko sasa Dhuhr baada ya kunuia kisha baada ya hapo aswali ´Aswr kutokana na ulazima wa kupangilia swalah. Mpangilio wa swalah hauanguki kwa mtu kuchelea kupitwa na swalah ya mkusanyiko. Kuhusu maneno ya wanazuoni (Rahimahumu Allaah):

“Akichelea kutoka nje wakati wa ile swalah ya sasa basi unaanguka mpangilio wa swalah.”

maana yake ni kwamba ni lazima kwa ambaye anadaiwa swalah iliyompita aianze kabla ya ile swalah ya sasa. Ukiwa ni mfinyu ule wakati wa swalah ya sasa basi ataanza ile swalah ya sasa. Mfano wa hilo mtu hajaswali swalah ya ´Ishaa na akaikumbuka wakati jua lilipokaribia kuchomoza na hajaswali Fajr ya siku hiyo, basi katika hali hiyo ataanza kuswali Fajr kabla ya kuondoka wakati wake. Kwa sababu wakati umemlazimikia. Baada ya hapo ndio ataswali ile swalah iliyompita.

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fataawaa Muhimmah, uk. 09-10
  • Imechapishwa: 10/08/2022