23 – Abu ´Umar bin Muhammad bin Ibraahiym bin Hakiym, mtumwa wa Banuu Haashim, ametukhabarisha: Muhammad bin Ibraahiym bin Muslim Abu Umayyah ametuhadithia: Abu Nu´aym al-Fadhwl bin Dukayn ametuhadithia: Hishaam bin Sa´d ametuhadithia, kutoka kwa Zayd bin Aslam, kutoka kwa Abu Swaalih, kutoka kwa Abu Hurayrah, aliyeeleza kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Wakati Allaah alipomuumba Aadam, alipangusa juu ya mgongo wake ambapo kikaanguka kutoka katika mgongo wake kila kizazi ambacho angekiumba mpaka siku ya Qiyaamah. Akaweka baina ya macho ya kila mtu miale ya nuru. Kisha Akawadhihirisha kwa Aadam ambaye alisema: ”Ee Mola, ni kina nani hawa?” Akasema: ”Hawa ni kizazi chako.” Kati ya wale watu akamuona bwana mmoja ambaye baina ya macho yake alikuwa na miale ya nuru na akasema: ”Ee Mola, huyu ni nani?” Akasema: ”Ni bwana mmoja kutoka katika ummah wako wa mwisho, anaitwa Daawuud.” Akasema: ”Ee Mola, ni muda kiasi gani Utamfanya kuishi?” Akasema: ”Miaka sitini.” Akasema: ”Ee Mola! Mzidishie miaka arobaini kutoka katika miaka yangu.” Wakati umri wa Aadam ulipomalizika, alikuja Malaika wa kifo. Akasema: ”Si nimebakiza katika umri wangu miaka arobaini?” Akasema: ”Je, si ulimpa Daawuud?” Aadam akakanusha na kizazi chake pia wakapinga. Aadam akasahau na kizazi chake pia kikasahau. Aadam akakosea na kizazi chake pia kikakosea.”

Hadiyth hii ni Swahiyh kutoka kwa Hishaam bin Sa´d, kutoka kwa Zayd bin Aslam, kutoka kwa Abu Swaalih, kutoka kwa Abu Hurayrah. Ameipokea Khalad na wengineo. Hadiyth hiyo imepokelewa pia na Swafwaan kutoka kwa ´Iysaa, kutoka kwa al-Haarith bin Abiy Dhubaab, kutoka kwa Sa´iyd al-Maqburiy, kutoka kwa Abu Hurayrah, kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Ni Swahiyh pia. ´Abdur-Rahmaan bin Zayd bin Aslam pia ameipokea kutoka kwa baba yake, kutoka kwa ´Atwaa’ bin Yasaar, kutoka kwa Abu Hurayrah.

  • Muhusika: Imaam Muhammad bin Ishaaq bin Mandah (afk. 395)
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ar-Radd ´alaal-Jahmiyyah, uk. 49-50
  • Imechapishwa: 09/06/2026
  • Taaliki: ´Allaamah ´Aliy bin Naaswir al-Faqiyhiy