Mambo yanapaswa kuwa namna hii na ni wajibu kwa wanafunzi na walinganizi kulitilia umuhimu jambo hili na wafanye kulingania katika Tawhiyd na kukemea shirki na kutokomeza shubuha ndio yenye kushika msitari wa mbele kabisa katika Da´wah yao. Huu ndio wajibu na hii ndio Da´wah ya Mitume (Swalla Allaahu ´alayhim wa sallam). Kila kitu ni chepesi kuliko shirki.

Ni vipi utakataza mambo mengine midhali bado kuna shirki? Ni lazima kwetu kuanza kwanza kukataza shirki na kuwasafisha waislamu kutokamana na hizi ´Aqiydh za kipindi cha kishirikina. Tunatakiwa kuwabainishia dalili na hoja na ikiwezekana kupambana nao Jihaad katika njia ya Allaah mpaka waislamu waweze kumpwekesha Allaah pekee katika ´ibaadah kadri na uwezo. Haya yanahusu kila zama na pahali. Haitakikani kwa wanafunzi wakaghafilika na jamob hili na badala yake wakaenda kutilia umuhimu na kutumia juhudi zao katika mambo mengine na wakawafumbia watu macho ambao wanatumbukia katika shirki na kuyaabudu makaburi ilihali makhurafi na mashaytwaan wa Suufiyyah wamezitawala akili za watu. Hili ni jambo ambalo haijuzu kulinyamazia. Kila Da´wah isiyokataza shirki basi hiyo ni Da´wah pungufu, isiyokuwa ya sawa na isiyozalisha matunda.

Vilevile ni wajibu kutambua kuwa kukiri Tawhiyd-ur-Rubuubiyyah haitoshi na wala hakunufaishi isipokuwa mpaka kuwe kumeambatana na kuikubali Tawhiyd-ul-Uluuhiyyah na kuihakikisha kimaneno, kivitendo na kiimani. Kadhalika inatakiwa kutambua kuwa washirikina waliotumiwa Mtume wetu Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhim wa sallam) walikuwa ni wenye kuikubali Tawhiyd-ur-Rubuubiyyah. Lakini pamoja na hivyo hakukuwafaa kitu kwa sababu walikuwa wakiikanusha Tawhiyd-ul-Uluuhiyyah.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Kashf-ish-Shubuhaat, uk. 15-16
  • Imechapishwa: 08/10/2016