08. Unywaji pombe wa hapa duniani unamzuia mtu kunywa pombe huko Aakhirah

D- Unywaji pombe wa hapa duniani unamzuia mtu kunywa pombe huko Aakhirah. Ibn ´Umar (Radhiya Allaahu ´anhumaa) ameeleza kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Yule mwenye kunywa pombe duniani basi hatoinywa huko Aakhirah.”[1]

Katika upokezi mwingine imekuja:

“Yule mwenye kunywa pombe duniani na akafa ilihali ni mwenye kuendelea, basi hatoinywa huko Aakhirah.”[2]

Katika upokezi mwingine imekuja:

“Yule mwenye kunywa pombe duniani na asitubu, basi hatoinywa huko Aakhirah.”[3]

an-Nasaa´iy na Ibn Maajah wana ziada kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh):

“Kisha Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: “Ni kinywaji cha watu wa Peponi. Yule mwenye kuacha kuinywa basi atainywa huko Aakhirah.”[4]

Abu Umaamah (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mola wangu ameapa kwa ufalme Wake: Mja Wangu hatoiacha kutokana na khofu yake Kwangu mimi isipokuwa nitamnywesha kutoka kwenye ghalani ya bustani.”[5]

Imaam al-Ismaa´iyliy ameipokea kupitia kwa ´Aliy na akazidisha:

“Watu wa Peponi wataiendea na wainywe. Allaah atawakirimu kwa hilo.”

Bi maana watakusanyika kwenye ghalani ya bustani wakinywa pombe.

´Abdullaah bin ´Amr (Radhiya Allaahu ´anhumaa) amesema:

“Katika Tawraat imekuja: “Yule mwenye kuinywa baada ya kuiharamisha basi nitamnywesha kutoka kwenye ghalani ya bustani.”[6]

Hivi sio kosa kubwa mtu akaharakisha kunywa kinywaji hichi kibaya kinachoiharibu akili na dini pamoja na kundi la mafusaki, watu duni na watu mashetani, na kuipa kipaumbele juu ya pombe iliosafi ambayo ni yenye ladha kwa wanywaji kwenye ghalani ya bustani pamoja na wale walioneemeshwa na Allaah – miongoni mwa Mitume, wakweli, mashahidi na waja wema?

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliota usingizini:

“Niliwaona watu watatu wakinywa pombe na wakiimba ambapo nikauliza ni kina nani. Wakasema: “Hawa ni Zayd bin Haarithah, Ja´far na ´Abdullaah bin Rawaahah.” Akawageukia na kuwatolea salamu. Hapo ilikuwa baada ya wao kufa mashahidi katika vita vya Mu´tah.”[7]

[1] al-Bukhaariy (5253) na Muslim (2003).

[2] Muslim (2003).

[3] al-Bukhaariy (5253).

[4] an-Nasaa’iy (6869) na Ibn Maajah (3374).

[5] Ahmad (5/257).

[6] al-Bayhaqiy katika ”as-Sunan al-Kubraa” (10/222) na al-Khatwiyb katika ”Muwadhdhwih Awhaam-il-Jam´ wat-Tafriyq” (2/159).

[7] at-Twabaraaniy katika ”al-Mu´jam al-Kabiyr” (7666).

  • Mhusika: Imaam Zayn-ud-Diyn bin Rajab al-Hanbaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Dhamm-ul-Khamr, uk. 18-20
  • Imechapishwa: 22/07/2020