08. Subira juu ya mtihani unaohusu watoto

Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Mtu anakuwa na nafasi mbele ya Allaah ambayo haifikiwi kwa matendo, ambapo Allaah anaendelea kumjaribu kwa anayoyachukia mpaka akaifikia.”[1]

Ameipokea Abu Ya´laa na kupitia kwake Ibn Hibbaan katika ”as-Swahiyh” yake.

Buraydah al-Aslamiy (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia kuwa amemsikia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akisema:

”Hakuna muislamu yeyote anayefikwa na janga lolote – mpaka akataja mwiba – isipokuwa kumekusudiwa moja katika mambo mawili; ima ni kwa sababu Allaah amsamehe dhambi ambayo asingemsamehe kwa jambo jengine au apate hadhi ambayo asingeipata kwa jambo jengine.”[2]

Ameipokea Abu Bakr bin Abiyd-Dunyaa.

Abul-Maliyh amesema: Muhammad bin Khaalid as-Sulamiy ametuhadithia, kutoka kwa baba yake, kutoka kwa baba yake (ambaye alikuwa Swahabah) aliyesema:

”Alitoka kwa ajili ya kumtembelea mmoja katika ndugu zake. Kabla ya kumfikia, akafikiwa na khabari kuwa amegonjweka. Akasema: ”Nimekuja kukuzuru, kukutembelea na kukupa bishara.” Akasema: ”Vipi umeyakusanya hayo?” Akasema: ”Nimetoka kwa lengo la kukutembelea, nikafikiwa na khabari kuwa unaumwa, ambapo ikawa kukutembelea. Aidha nitakupa bishara ya jambo nililolisikia kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akilisema: ”Ikiwa imeshahukumiwa kwa mja kupata nafasi mbele ya Allaah ambayo hawezi kuifikia kwa matendo yake, basi Allaah (´Azza wa Jall) humpa mtihani katika mwili wake, mtoto wake au katika mali yake ambapo akamfanya kusubiri mpaka akaweza kufikia ngazi ambayo Allaah (´Azza wa Jall) alikuwa amekwishaiamua.”[3]

Mitihani juu ya watoto ni miongoni mwa majaribio makubwa na mabalaa mazito. Ni moto unaowashwa ndani ya moyo na ni maumivu yanayochoma kwenye maini. Ndio maana thawabu za mwenye kusubiri juu ya jambo hilo zikawa kubwa na ujira wake kwenye mizani yake siku ya Qiyaamah ukawa mzito. an-Nasaa´iy amepokea kutoka kwa Abu Salmaa (Radhiya Allaahu ´anh), mchunga wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), aliyemsikia Mtume wa Allaah  (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akisema:

”Hongera kwa mambo matano yana uzito kiasi gani kwenye mizani:

لا إله إلا الله و سبحان الله والحمد لله والله أكبر

”Hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah, Allaah ametakasika kutokana na mapungufu, himdi zote njema ni stahiki ya Allaah na Allaah ni mkubwa.”

Muislamu anafiwa na mtoto mwema na akataraji malipo kutoka kwa Allaah.”[4]

Ameipokea Ibn Hibbaan katika “as-Swahiyh” yake, al-Haakim, ambaye ameisahihisha, katika “al-Mustadrak” na at-Twabaraaniy katika “al-Mu´jam al-Kabiyr”. al-Bazzaar ameipokea katika “al-Musnad” yake kupitia kwa Thawbaan kwa cheni ya wapokezi nzuri. at-Twabaraaniy ameipokea katika “al-Mu´jam al-Awsatw” yake kupitia kwa Safiynah kwa cheni ya wapokezi nzuri.

[1] Abu Ya´laa (6095), Ibn Hibbaan (2897) na al-Bayhaqiy katika “al-Adab” (1048).

[2] Abu Nu´aym (6833) na ad-Daylamiy katika “al-Firdaws” (6229). Cheni ya wapokezi ni dhaifu kwa mujibu wa al-Albaaniy katika “as-Swahiyhah” (6/192).

[3] Abu Daawuud (3090) na Ahmad (5/272). Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy “Swahiyh Sunan Abiy Daawuud” (3090).

[4] an-Nasaa’iy katika “´Amal-ul-Yawm wal-Laylah” (167), Ibn Hibbaan (2328), at-Twabaraaniy (873) na al-Haakim (1/511-512). Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika “as-Swahiyhah” (1204).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin ´Abdillaah bin Naaswir-id-Diyn ad-Dimashqiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Bard-ul-Akbaad ´inda Faqd-il-Awlaad, uk. 45-49
  • Imechapishwa: 13/08/2023