07. Mitihani inafuta madhambi ya muislamu

Zipo Hadiyth nyingi na zilizo wazi zinazotilia nguvu namna ambavyo ambaye amepatwa na msiba analipwa thawabu na kurehemewa. Miongoni mwazo ni yale aliyopokea al-Bukhaariy na wengineo ya kwamba Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Yule ambaye Allaah anamtakia kheri basi humpa msiba.”[1]

Umm Salamah (Radhiya Allaahu ´anhaa) ameeleza kuwa amemsikia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akisema:

”Allaah hajampa mja mtihani kwa njia ambayo anaichukia, isipokuwa Allaah hufanya mtihani huo ukawa ni kafara na kusafika muda wa kuwa hajayafanya majaribio yaliyompata kwa mwengine asiyekuwa Allaah au akamuomba mwengine asiyekuwa Allaah katika kuuondosha.”[2]

Ameipokea Abu Bakr Abiy Abiyd-Dunyaa (Rahimahu Allaah) katika “al-Maradhw wal-Kaffaaraat”.

Sa´d bin Abiy Waqqaas (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

”Nilisema: ”Ee Mtume wa Allaah! Ni watu gani wenye mitihani mikubwa zaidi?” Akasema: ”Ni Mitume. Kisha wanaowafuatia, kisha wanaowafuatia. Mtu hupewa mtihani kutegemea [na nguvu ya] dini yake. Jinsi ambavyo dini yake inakuwa madhubuti ndivo mtihani wake unakuwa mkubwa zaidi. Na ikiwa dini yake ina ulaini basi hupewa mitihani kwa kiasi cha dini yake. Mitihani haimwachi mja mpake pale anapotembea juu ya ardhi hali ya kuwa hana dhambi.”[3]

Ameipokea at-Tirmidhiy, an-Nasaa’iy, Ibn Maajah na Ibn Abiyd-Dunyaa na imesahihishwa na at-Tirmidhiy. Imepokelewa vilevile na Abu Haatim katika ”as-Swahiyh” kwa tamko lisemalo:

”Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliulizwa: ”Ni watu gani wenye mitihani mikubwa zaidi?” Akasema: ”Ni Mitume. Kisha wanaowafuatia, kisha wanaowafuatia. Mtu hupewa mtihani kutegemea [na nguvu ya] dini yake. Ambaye dini yake ni madhubuti zaidi ndivo mtihani wake unakuwa mkubwa zaidi, na ambaye dini yake ina ulaini basi hupewa mtihani mwepesi. Mtu ataendelea kusibiwa na mitihani mpaka atembee kati ya watu hali kuwa hana dhambi.”

Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza kuwa amemsikia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akisema:

”Mitihani haiachi kumpata muumini wa kiume na muumini wa kike katika nafsi yake, watoto wake na mali yake, mpaka akutane na Allaah ilihali hana madhambi.”[4]

Ameipokea at-Tirmidhiy na al-Haakim na ameisahihisha.

Abu Sa´iyd al-Khudriy (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Hakuna muislamu anayepatwa na kutaabika, uzito, maradhi, huzuni, maudhi, dhiki mpaka ule mwiba unaomchoma isipokuwa Allaah humfutia dhambi zake kwayo.”[5]

Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim.

Anas (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

”Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuja na mti ambapo akautikisa mpaka yakadondoka majani yake. Kisha akasema: ”Misiba na maumivu yanaharakisha madhambi ya mwanadamu zaidi kuliko mimi ninavoufanya mti huu.”[6]

Ameipokea Abu Ya´laa al-Mawsiliy katika “al-Musnad” na Ibn Abiyd-Dunyaa.

[1] al-Bukhaariy (5645) na Ahmad (2/237).

[2] al-Maradh wal-Kaffaaraat (43) na (205). Nzuri kwa mujibu wa al-Albaaniy katika “Swahiyh-ut-Targhiyb wat-Tarhiyb” (3401).

[3] at-Tirmidhiy (2398), Ibn Maajah (4023), Ahmad (1/172), Ibn Hibbaan (2900), al-Haakim (121) na al-Bayhaqiy (6326). Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Swahiyh-ul-Jaamiy´” (994).

[4] at-Tirmidhiy (2399) na al-Haakim (1/346). Nzuri na Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika “Swahiyh Sunan at-Tirmidhiy” (2399).

[5] al-Bukhaariy (5641-5642) na Muslim (2573).

[6] Abu Ya´laa (4299) na Ibn Abiyd-Dunyaa katika “al-Maradhw wal-Kaffaaraat” (57) na (88). Dhaifu kwa mujibu wa al-Albaaniy katika “al-Mutafarriqaat” (261).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin ´Abdillaah bin Naaswir-id-Diyn ad-Dimashqiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Bard-ul-Akbaad ´inda Faqd-il-Awlaad, uk. 40-45
  • Imechapishwa: 13/08/2023