06. Ufanye msiba wako kuwa furaha

Tumesimuliwa kuwa wakati al-Hasan bin al-Hasan bin ´Aliy alipofariki, mwanamke wake aliweka hema karibu na kaburi lake kwa kipindi cha mwaka kisha baadaye akaliondosha. Ndipo wakasikia sauti ikisema:

”Je, wamepata kile walichopoteza? Ndipo akajibu mwengine: ”Bali wamekata tamaa wakarudi.”[1]

Ameipokea al-Bukhaariy katika ”as-Swahiyh” yake kwa cheni ya wapokezi pungufu.

Imekuja katika upokezi mwingine:

”Wakati alipofarijika na hema likaondoshwa, walisikia sauti pasi na kuona inatokea kwa wapi: ”Kidirikini mlichopoteza!” Ndipo akasema mwingine: ”Bali wamekata tamaa ndio wakaondoka.”

Zipo Hadiyth nyingi zinazotaja subira na fadhilah zake ambapo tunatosheka na baadhi tu ya hizi chache. Maana ya subira kilugha ni kujizuilia. Subira ina nguzo tatu:

1 – Kuizuia nafsi kutokasirikia hukumu ya Allaah.

2 – Kuzuia ulimi kuzungumza maneno mabaya na machafu.

3 – Kuzuia viungo vya mwili kutokana na maasi, kama kujipiga mashavu, kupasua nguo na kuchora rangi nyeusi maeneo pa wazi.

Mtu akitekeleza nguzo hizi tatu basi anapata fadhilah za subira – subira ambayo ndio nusu ya imani. Isitoshe mtihani wake unageuka kuwa mkubwa na zawadi kubwa, na yanakuwa yale aliyokuwa akiyachukia yenye kupendeza. Aidha analipwa thawabu nyingi. Abu Dharr (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Kuipa nyongo dunia inahusiana na kutotegemea yale yaliyomo mkononi mwako zaidi kuliko unavyotegemea yaliyomo mkononi mwa Allaah, na kwamba upendelee zaidi thawabu juu ya msiba uliyokupata kuliko endapo ungekukosa.”[2]

´Alqamah ameeleza kuwa ´Abdullaah bin Mas´uud (Radhiya Allaahu ´anh) amesema kuhusiana na maneno ya Allaah (Tabaarak wa Ta´ala):

مَا أَصَابَ مِن مُّصِيبَةٍ إِلَّا بِإِذْنِ اللَّـهِ ۗ وَمَن يُؤْمِن بِاللَّـهِ يَهْدِ قَلْبَهُ ۚ وَاللَّـهُ بِكُلِّ شَيْءٍ عَلِيمٌ

“Hausibu msiba wowote [kukupateni] isipokuwa kwa idhini ya Allaah. Yeyote   anayemuamini Allaah, basi huuongoza moyo wake. – Allaah kwa kila kitu ni mjuzi.”[3]

”Inahusiana na msiba uliyompata mtu ambapo akajua kuwa ni wenye kutoka kwa Allaah na hivyo akajisalimisha nao na kuridhia.”

al-Bukhaariy amepokea mfano wake katika ”as-Swahiyh” yake kwa cheni ya wapokezi pungufu kutoka kwa ´Alqamah.

Umm-ud-Dardaa´ (Radhiya Allaahu ´anhaa) amesema:

”Wale wanaoridhia maamuzi ya Allaah ni wale wanaoridhia chochote Anachowahukumia. Peponi watakuwa na ngazi ambazo watahusudiwa na mashahidi.”[4]

Ahmad bin Abiyl-Hawaariy amesema: Muhammad bin Ja´far bin Muhammad amenihadithia:

”Walimweleza Rabiy´ah kuhusu mfanya ´ibaadah mmoja wa wana wa israaiyl ambaye alikuwa hali kwa mwaka isipokuwa mara moja tu. Anaondoka mahali pake pa kufanya ´ibaadah na kwenda katika rundo la takataka nje ya mlango wa mfalme ili kuokoka mabaki ya chakula chake. Bwana mmoja alikuwa karibu naye akasema: ”Ni kipi kingemdhuru, kwa kuzingatia pia nafasi aliokuwa nayo, angemuomba Allaah kumjaalia riziki yake kwa njia nyingine mbali na hii?” Ndipo Rabiy´ah akasema: ”Ole wako! Hakika mawalii wa Allaah hawakasiriki kwa yale ambayo Allaah amewahukumia.”[5]

[1] Tazama “Fath-ul-Baariy” (3/200).

[2] at-Tirmidhiy (2340) aliyesema kuwa ni ngeni. Dhaifu mno kwa mujibu wa al-Albaaniy katika “Dhwa´iyf Sunan at-Tirmidhiy” (2340).

[3] 64:11

[4] ar-Ridhwaa ´an-il-Laah wa Qadhwaa-ih (8) ya Ibn Abiyd-Dunyaa.

[5] ar-Ridhwaa ´an-il-Laah wa Qadhwaa-ih (21).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin ´Abdillaah bin Naaswir-id-Diyn ad-Dimashqiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Bard-ul-Akbaad ´inda Faqd-il-Awlaad, uk. 37-40
  • Imechapishwa: 13/08/2023