08. Picha iliyoharamishwa kwa mujibu wa Shari´ah

Katika Hadiyth ya Abu Hurayrah kumekwishatangulia mafahamisho juu ya kwamba picha inafaa kuiacha nyumbani pale kinapokatwa kichwa chake. Kwa sababu inakuwa katika maumbile ya mti. Isitoshe hayo yanafahamisha pia kuwa kuchukua picha ya mti na venginevyo visivyokuwa na roho ni kitu kinachofaa. Hayo yametangulia kwa uwazi katika upokezi wa al-Bukhaariy na Muslim unaotokamana na Ibn ´Abbaas.

Hadiyth inayokusudiwa inafahamisha pia kuwa haitoshi kukata kisichokuwa kichwa kutoka katika picha kama vile kukata nusu yake kwa chini na mfano wake. Vilevile picha kama hiyo hairuhusiwi kuitumia na wala hakuondoki kikwazo cha kuingia kwa Malaika. Kwa sababu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliamrishwa kuiharibu na kuifuta picha hiyo na akaeleza kuwa inazuia kuingia kwa Malaika. Isipokuwa zile picha zinazotwezwa au zikakatwa kichwa chake. Yeyote atakayedai kufaa kubaki nyumbani picha – mbali na picha aina mbili hizi – basi analazimika kuleta dalili kutoka ndani ya Qur-aan na Sunnah.

Jengine ni kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ameeleza kuwa picha kinapokatwa kichwa chake basi kubaki kwake kunakuwa kama umbo la mti. Hayo yanajulisha kuwa kinachojuzisha kufaa kubaki kwake ni pale inapotoka nje ya umbo la viumbe vyenye roho na badala yake ikafanana na viumbe visivyokuwa na uhai. Picha inapokatwa sehemu yake ya chini na kukabaki kichwa chake haiwi katika sifa hiyo kwa kule kubakia uso. Sababu nyingine ni kuwa uanzilishi wa maumbile unaanza usoni na picha haizingatiwi katika viungo vyengine vya mwili vilivyobakia. Kwa hiyo kwa yule anayeelewa makusudio ya Allaah na Mtume Wake basi haijuzu kulinganisha picha ilio na kichwa juu ya isiyokuwa na kichwa.

Kwa ajili hiyo inamdhihirikia yule anayetafuta haki kwamba kuchukua picha kichwa na vinavyofuatia katika wanyama ni mambo yanaingia katika uharamu na makatazo. Kwa sababu Hadiyth ambazo ni Swahiyh zilizotangulia zinajumuisha na kichwa. Haifai kwa yeyote kubagua kutoka katika kuenea kwake isipokuwa yale yaliyobaguliwa na Shari´ah.

Hakuna tofauti katika haya kati ya picha zenye kiwiliwili wala nyenginezo zilizofanyiwa nakshi katika pazia, karatasi au chengine mfano wavyo. Wala hakuna tofauti kati ya picha za wanaadamu na viumbe vyengine vyote vilivyo na roho. Wala hakuna tofauti kati ya picha za wanazuoni, viongozi na wengineo. Bali uharamu wa picha za viongozi, wanazuoni na wengineo katika wale wanaotukuzwa ni mkubwa zaidi. Kwa sababu ni kukubwa zaidi kupewa mtihani kwazo. Kusimamisha picha zao katika vikao na kwenginepo na kuzitukuza ni miongoni mwa aina kubwa ya njia inayopelekea katika shirki na kuabudiwa wale mabwana wa picha hizo badala ya Allaah. Hayo yalitokea kwa watu wa Nuuh. Katika maneno ya al-Khattwaabiy kumetangulia kuashiria jambo hilo.

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Jawaab al-Mufiyd fiy Hukm-it-Taswwiyr kutoka katika Majmuu´-ul-Fataawaa (04/218-219)
  • Imechapishwa: 28/03/2022