08. Msomi ni mwenye kuona na mjinga ni kipofu

Wale waliochagua njia ya elimu tukufu wamejichagulia wenyewe – baada ya fadhilah na neema za Allaah juu yao – njia bora, kitendo chema na takasifu zaidi. Kwa sababu hakuna yeyote awezaye kuyafanya vizuri zaidi matendo yake isipokuwa mpaka aitangulizie elimu. Makusudio ni ile elimu ya dini yenye kuchotwa kutoka katika Qur-aan na Sunnah. Ummah wanatakiwa kumpata mtu wa kuwazindua juu ya hilo, kuwasaidia juu ya hilo, kuziweka juhudi zake ndani ya juhudi zao ima kwa njia ya kufunza, kuelekeza katika jambo la kheri na kuvutia katika fadhilah na utukufu huu mkubwa. Inatosha Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) kuitukuza elimu na wanachuoni:

إِنَّمَا يَخْشَى اللَّـهَ مِنْ عِبَادِهِ الْعُلَمَاءُ

“Hakika si vyenginevyo wanaomkhofu Allaah miongoni mwa waja Wake ni wanazuoni.”[1]

يَرْفَعِ اللَّـهُ الَّذِينَ آمَنُوا مِنكُمْ وَالَّذِينَ أُوتُوا الْعِلْمَ دَرَجَاتٍ

“Allaah atawainua wale walioamini miongoni mwenu na waliopewa elimu daraja za juu zaidi.”[2]

Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) amemzingatia msomi kuwa ni muoni na mjinga kuwa ni kipofu pale aliposema (´Azza wa Jall):

أَفَمَن يَعْلَمُ أَنَّمَا أُنزِلَ إِلَيْكَ مِن رَّبِّكَ الْحَقُّ كَمَنْ هُوَ أَعْمَىٰ ۚ إِنَّمَا يَتَذَكَّرُ أُولُو الْأَلْبَابِ

“Je, anayejua kwamba yaliyoteremshwa kwako kutoka kwa Mola wako ni haki [na akayafuata je analingana] kama aliyekuwa kipofu? Hakika wanazingatia wenye akili tu.”[3]

Tazama tofauti hii ya wazi kati ya msomi mwenye kuona na mjinga ambaye anahangaika katika dunia hii; akifanya matendo hawezi kupambanua kati ya yaliyo ya sawa na yaliyo ya makosa, yaliyo sahihi na yasiyokuwa sahihi. Hayo si kwa sababu nyengine isipokuwa ujinga ambao sababu yake ni mtu kujiweka mbali na vikao vya elimu na halaqa za wanachuoni walezi.

Miongoni mwa yale yaliyopokelewa yanayovutia katika elimu inayozalisha matendo mema ni maneno ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Yeyote atakayefuta njia akifuta elimu ndani yake, basi Allaah atamfanyia wepesi njia ya kuelekea Peponi.”

Katika upokezi mwingine imekuja:

“… basi Allaah atamfanyia wepesi njia ya kuelekea Peponi.”[4]

Ahadi hii tukufu Allaah amewatofautisha kwayo wale wenye kupita katika njia ya elimu. Wale ambao wanatafuta elimu yenye manufaa ambayo inazalisha matendo mema ambayo wanatarajia nyuma yake radhi za Allaah na Pepo Yake katika Nyumba Yake Peponi na wakati huohuo wanaiogopa adhabu Yake iumizayo. Muumini siku zote anakuwa kati ya khofu na matarajio.

Kwa hivyo watu wanapaswa kuitendea kazi elimu. Kwani ndio matunda yake. Mja akijifunza kitu na akakitendea kazi basi elimu yake haitimii isipokuwa kwa kuwalingania wengine ili wajue nao watendee kazi kwa kiasi cha uwezo wake na upeo wa juhudi zake kwa wale ndugu na wasiokuwa ndugu. Ingawa wale ndugu zake wana haki zaidi ya kulinganiwa:

وَأَنذِرْ عَشِيرَتَكَ الْأَقْرَبِينَ

“Na waonye jamaa zako wa karibu.”[5]

[1] 35:28

[2] 58:11

[3] 13:19

[4] Abu Daawuud (03/316), at-Tirmidhiy (07/374) na Ibn Maajah (01/81). Ni Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika “Swahiyh Sunan Ibn Maajah” (01/43).

[5] 26:214

  • Mhusika: ´Allaamah Zayd bin Muhammad al-Madkhaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Twariyqal-Usuwl ilaa idhwaah-ith-Thalaat-il-Usuwl, uk. 23-24
  • Imechapishwa: 22/11/2021