07. Ulazima wa mtu kufanyia kazi yale aliyojifunza

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Suala la pili: Kuifanyia kazi.

MAELEZO

Bi maana elimu hiyo. Haya ni miongoni mwa mambo muhimu. Kwa sababu matendo ndio matunda ya elimu. Yule mwenye kujua na asiitendee kazi elimu yake anapata dhambi. Ameiweka nafsi yake mwenyewe katika khatari kubwa mno, kama mfano wa mayahudi na wale wenye kujifananisha nao, na kitendo chake kinapelekea katika matishio makubwa kabisa. Kwa ajili hiyo wanachuoni wetu (Rahimahumu Allaah) wamesema:

“Mwenye kuharibika katika wasomi wetu ana ufanano na mayahudi. Mwenye kuharibika katika wafanyaji ´ibaadah wetu ana ufanano na wakristo.”[1]

Ubainifu wa hayo ni kwamba Allaah amewateremshia mayahudi elimu yenye manufaa ambayo ni Tawraat. Ndani yake mna uongofu na nuru. Wakaipotosha na kubadilisha. Kwa sababu hawakutaka kuyatendea kazi maandiko ya Tawraat kama ambavo Allaah aliyateremsha kwa Muusa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Hivyo wakaharibika na wakastahiki hasira kutoka kwa Allaah (´Azza wa Jall). Matokeo yake Allaah akawakasirikia kwa sababu walijua na hawakutendea kazi. Kwa ajili hiyo yule atakayejua katika Ummah wa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) chochote kutoka katika mafunzo ya Qur-aan na Sunnah na asikitendee kazi, basi amejifananisha na wale waliokasirikiwa. Imepokelewa katika Hadiyth:

“Yule atakayejifananisha na watu basi yeye ni katika wao.”[2]

Maana yake ni kwamba anastahiki kuadhibiwa kama wao walivyostahiki kuadhibiwa. Adhabu ya kila mfanya jinai ni kutegemea na jarima yake na alivyoifanyia nafsi yake mwenyewe jinai.

Kwa hivyo kilicho cha lazima kwa muislamu aifuatishie elimu matendo. Kila pale atapofahamu masuala fulani miongoni mwa masuala ya Uislamu ayatendee kazi ili aweze kupata thawabu nyingi, atekeleze faradhi, atekeleze mambo ya wajibu na ajiepushe na mambo yaliyo ya haramu. Matendo yote hayo sababu yake ni elimu. Elimu ni ufunguo wa wema wote na ni mlango wa kheri zote. Mwenye kunyimwa elimu amenyimwa kheri zote. Kwa sababu Allaah (´Azza wa Jall) amewatuma Mitume kwa elimu na ameteremsha vitabu kwa elimu. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Wanachuoni ni warithi wa Mitume. Hakika Mitume hawarithishi dinari wala dirhamu. Lakini wanachorithisha ni elimu. Mwenye kuinyakua basi amejinyakulia fungu kubwa.”[3]

Elimu inayozalisha matendo mema mtu – ni mamoja mwanamume au mwanamke – haipati isipokuwa akifanya bidii katika kuitafuta, akawa na nia nzuri na waislamu wa kiume na wa kike wakaitilia umuhimu. Kwa kiasi cha mtu atavyofanya bidii ndivo atavyoipata elimu na kuichuma. Kuhusu kufanya uvivu, kuitii nafsi katika mambo ya matamanio, pumbao na michezo ni miongoni mwa sababu za mtu kunyimwa. Nafsi, ni kama Allaah alivyoisifu, ni yenye kuamrisha sana maovu.

[1] Yametajwa na Ibn Taymiyyah kutoka kwa Ibn ´Uyaynah na wengineo katika “Iqtidhwaa´-us-Swiraatw al-Mustaqiym” (01/67). Vilevile Ibn Kathiyr katika “Tafsiyr” yake (02/351) na al-Munaawiy katika “Faydw al-Qadiyr” (05/261).

[2] Abu Daawuud (04/44).

[3] Abu Daawuud (03/316), at-Tirmidhiy (07/374) na Ibn Maajah (01/81). Ni Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika “Swahiyh Sunan Ibn Maajah” (01/43).

  • Mhusika: ´Allaamah Zayd bin Muhammad al-Madkhaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Twariyqal-Usuwl ilaa idhwaah-ith-Thalaat-il-Usuwl, uk. 21-23
  • Imechapishwa: 22/11/2021