Ni kuamini kwa kukata na kusadikisha ya kwamba Allaah (Ta´ala) ametumilizia watu Mitume na akawateremshia Wahy. Mitume hao wanawalingania watu na kuwaelekeza katika yale waliyoumbiwa kwayo ambayo ni kumwabudu Yeye pekee na kumtii. Aidha wanawabainishia njia ya uokozi na kuwahimiza kwayo na sambamba na hilo wanawatahadharisha na njia ya maangamivu. Vilevile wale wenye kuwatii wanawabashiria Pepo na wanawaonya Moto wale wenye kuwaasi. Hoja ya Allaah juu ya viumbe Wake imesimama kwa kutumilizwa Mitume na zimekatika nyudhuru zao. Amesema (Ta´ala):

رُّسُلًا مُّبَشِّرِينَ وَمُنذِرِينَ لِئَلَّا يَكُونَ لِلنَّاسِ عَلَى اللَّـهِ حُجَّةٌ بَعْدَ الرُّسُلِ

“Mitume wenye kutoa bishara njema na waonyaji ili pasikuweko kutoka kwa watu hoja yoyote juu ya Allaah baada ya kuletwa ya Mitume.”[1]

Tunawaamini Mitume kwa ujumla na kwamba Allaah amewatuma Mitume wengi ili kuwaongoza watu. Tunawaamini kwa upambanuzi wale ambao Allaah amewataja ndani ya Kitabu Chake au Mtume Wake ndani ya Sunnah zake. Amesema (Ta´ala):

إِنَّا أَوْحَيْنَا إِلَيْكَ كَمَا أَوْحَيْنَا إِلَىٰ نُوحٍ وَالنَّبِيِّينَ مِن بَعْدِهِ ۚ وَأَوْحَيْنَا إِلَىٰ إِبْرَاهِيمَ وَإِسْمَاعِيلَ وَإِسْحَاقَ وَيَعْقُوبَ وَالْأَسْبَاطِ وَعِيسَىٰ وَأَيُّوبَ وَيُونُسَ وَهَارُونَ وَسُلَيْمَانَ ۚ وَآتَيْنَا دَاوُودَ زَبُورًا وَرُسُلًا قَدْ قَصَصْنَاهُمْ عَلَيْكَ مِن قَبْلُ وَرُسُلًا لَّمْ نَقْصُصْهُمْ عَلَيْكَ ۚ وَكَلَّمَ اللَّـهُ مُوسَىٰ تَكْلِيمًا

“Hakika Tumekufunulia Wahy kama tumevyomfunulia Wahy Nuuh na Manabii baada yake na tumemfunulia Wahy Ibraahiym na Ismaa’iyl na Ishaaq na Ya’quub na vizazi na ‘Iysaa na Ayyuub na Yuunus na Haaruun na Sulaymaan, na tumempa Daawuud Zabuur. Na Mitume Tuliokwishakusimulia mikasa yao hapo kabla na Mitume wengine hatukukusimulia mikasa yao – na bila shaka Allaah alimzungumzisha Muusa maneno ya kweli.”[2]

Amesema (Ta´ala) katika Suurah al-An´am baada ya kumtaja Ibraahiym (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

وَوَهَبْنَا لَهُ إِسْحَاقَ وَيَعْقُوبَ ۚ كُلًّا هَدَيْنَا ۚ وَنُوحًا هَدَيْنَا مِن قَبْلُ ۖ وَمِن ذُرِّيَّتِهِ دَاوُودَ وَسُلَيْمَانَ وَأَيُّوبَ وَيُوسُفَ وَمُوسَىٰ وَهَارُونَ ۚ وَكَذَٰلِكَ نَجْزِي الْمُحْسِنِينَ وَزَكَرِيَّا وَيَحْيَىٰ وَعِيسَىٰ وَإِلْيَاسَ ۖ كُلٌّ مِّنَ الصَّالِحِينَ

“Tukamtunukia Ishaaq na Ya’quub – wote tuliwaongoza –  na Nuuh tulimwongoza kabla na katika dhuria wake [tuliwaongoza pia] Daawuud na Sulaymaan na Ayyuub na Yuusuf na Muusa na Haaruun – na hivyo ndivo tunawalipa wafanyao wema – na Zakariyyaa na Yahyaa na ‘Iysaa na Ilyaas – wote ni miongoni mwa waja wema.”[3]

[1] 04:165

[2] 04:163-165

[3] 06:84-85

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajihiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Iymaan – Haqiyqatuhu wa Nawaaqidhwuh, uk. 15-16
  • Imechapishwa: 21/03/2023