Wale Mitume watano wenye subira sana ndio bora zaidi. Nao ni Nuuh, Ibraahiym, Muusa, ´Iysaa na Muhammad (Swalla Allaahu ´alayim wa sallam). Wametajwa katika maneno Yake (Ta´ala) katika Suurah al-Ahzaab:

وَإِذْ أَخَذْنَا مِنَ النَّبِيِّينَ مِيثَاقَهُمْ وَمِنكَ وَمِن نُّوحٍ وَإِبْرَاهِيمَ وَمُوسَىٰ وَعِيسَى ابْنِ مَرْيَمَ ۖ وَأَخَذْنَا مِنْهُم مِّيثَاقًا غَلِيظًا

“Na wakati Tulipochukua kutoka kwa Manabii fungamano lao, na kutoka kwako na kutoka kwa Nuuh na Ibraahiym na Muusa na ‘Iysaa mwana wa Maryam na Tukachukua kutoka kwao fungamano gumu.”[1]

Vilevile maneno Yake (Ta´ala) katika Suurah ash-Shuuraa:

شَرَعَ لَكُم مِّنَ الدِّينِ مَا وَصَّىٰ بِهِ نُوحًا وَالَّذِي أَوْحَيْنَا إِلَيْكَ وَمَا وَصَّيْنَا بِهِ إِبْرَاهِيمَ وَمُوسَىٰ وَعِيسَىٰ ۖ أَنْ أَقِيمُوا الدِّينَ وَلَا تَتَفَرَّقُوا فِيهِ ۚ

“Amekuwekeeni katika dini yale aliyomuusia kwayo Nuuh na ambayo tumekuteremshia Wahy wewe na tuliyomuusia kwayo Ibraahiym na Muusa na ‘Iysaa kwamba: “Simamisheni dini na wala msifarikiane humo.”[2]

Wabora katika hao watano ni wapenzi wa Allaah wa wandani; Ibraahiym na Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhim wa sallam). Mbora katika wawili hao ni Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Yeye ni sehemu yetu katika Mitume na sisi ni sehemu yake katika ummah wake. Kwa hivyo ni lazima kumuamini (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), kumshuhudilia ujumbe, kumtii katika maamrisho yake, kumsadikisha katika maelezo yake, kujiepusha na makatazo yake na aliyokemea na kumwabudu Allaah kwa yale aliyoyawekea Shari´ah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Aidha ni lazima kuamini kuwa yeye ndiye Mtume wa mwisho. Amesema (Ta´ala):

مَّا كَانَ مُحَمَّدٌ أَبَا أَحَدٍ مِّن رِّجَالِكُمْ وَلَـٰكِن رَّسُولَ اللَّـهِ وَخَاتَمَ النَّبِيِّينَ

“Hakuwa Muhammad baba wa yeyote miongoni mwa wanaume wenu, lakini ni Mtume wa Allaah na ni mwisho wa Manabii.”[3]

Imekuja katika Hadiyth ambayo ni Swahiyh:

“Utume umekhitimishwa kwangu.”[4]

[1] 33:07

[2] 42:13

[3] 33:40

[4] Muslim (523).

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajihiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Iymaan – Haqiyqatuhu wa Nawaaqidhwuh, uk. 16-17
  • Imechapishwa: 21/03/2023