08. Maamrisho ya ash-Shaafi´iy ya kushikamana na Sunnah

3- ash-Shaafi´iy (Rahimahu Allaah)

Ama kuhusu Imaam ash-Shaafi´iy, maneno kutoka kwake ni mengi na mazuri[1] na wafuasi wake ambao waliyatendea kazi ni wengi. Amesema ikiwa ni pamoja na:

1- “Hakuna yeyote isipokuwa anapitwa na Sunnah za Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Maneno yoyote nitayosema au msingi wowote nitaoweka usioafikiana na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), basi maneno yatakayotumika ni yale ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Hayo yatakuwa ndio maoni yangu pia.”[2]

2- “Waislamu wameafikiana juu ya kwamba yule ambaye atabainikiwa na Sunnah ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), basi haifai kwake kuyaacha kwa sababu ya maoni ya mwengine.”[3]

3- “Mkisoma katika kitabu changu na kupata kitu kinachopingana na Sunnah za Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), basi ichukueni Sunnah ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na mwacheni na maoni yangu.”[4]

Katika upokezi mwingine imekuja:

“Mkisoma katika kitabu changu na kupata kitu kinachopingana na Sunnah za Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), basi ifuateni na mpuuze maneno ya mwengine.”[5]

4- “Itaposihi Hadiyth basi hayo ndio madhehebu yangu.”[6]

5- “Nyinyi[7] ni watambuzi zaidi wa Hadiyth na wanaume kuliko mimi. Hivyo basi, Hadiyth ikiwa ni Swahiyh nifunzeni nayo pasi na kujali ni yenye kutoka Kuufah, Baswrah au Shaam. Ili niichukue midhali ni Swahiyh.”

6- “Masuala yoyote ambayo kuna upokezi Swahiyh kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) yanayotofautiana na maoni yangu, basi mimi najirejea maoni yangu wakati uhai wangu na baada ya kufa kwangu.”[8]

7- “Mkinisikia nasema kitu ilihali kuna kingine kilichosihi kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), basi mtambue kuwa akili yangu imeniondoka.”[9]

8- “Kila nitakachokisema na wakati huohuo kukasihi kupokelewa kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kinachopingana na nilichokisema, basi Hadiyth ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ndio itakayotangulizwa. Kwa hivyo msinifuate kichwa mchunga.”[10]

9- “Kila Hadiyth kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ndio maoni yangu hata kama hukuisikia kutoka kwangu.”[11]

[1] Imaam Ibn Hazm amesema:

“Wanachuoni waliofuatwa walitupilia mbali kufuata kichwa mchunga na waliwakataza wanafunzi zao kuwafuata kipofu. Ambaye alikuwa mkali katika wao katika hilo ni ash-Shaafi´iy. Alitilia (Rahimahu Allaah) umuhimu mkubwa juu ya kufuata mapokezi Swahiyh na kuchukua dalili na akajitenga mbali juu ya kufuatwa kwa ujumla. Aliyasema hayo wazi. Allaah anufaishe kupitia kwake na ampe ujira mkubwa. Kwani yeye alikuwa ni sababu katika kheri nyingi.” (6/118).

[2] al-Haakim kwa cheni ya wapokezi Swahiyh mpaka kwa ash-Shaafi´, kama alivyotaja Ibn ´Asaakir katika ”Taariykh Dimashq” (3/1/15), I´laam-ul-Muwaqqi´iyn (2/363-364) na al-Iyqaadhw, uk. 100.

[3] Ibn-ul-Qayyim (2/361) na al-Fulaaniy, uk. 68.

[4] al-Harawiy katika ”Dhamm-ul-Kalaam” (1/47/3), al-Khatwiyb katika ”al-Ihtijaaj bish-Shaafi´iy” (2/8), Ibn ´Asaakir (1/9/15), an-Nawawiy katika ”al-Majmuu´” (1/63), Ibn-ul-Qayyim (3/361), al-Fulaaniy, uk. 100.

[5] Abu Nu´aym katika ”Hilyat-ul-Awliyaa’” (9/107) na Ibn Hibbaan katika ”as-Swahiyh” (3/284) kwa cheni ya wapokezi Swahiyh.

[6] an-Nawawiy katika marejeo yaliyotangulia, ash-Sha´raaniy (1/57) ambaye ameinasibisha kwa al-Haakim na al-Bayhaqiy na al-Fulaaniy, uk. 107. ash-Sha´raaniy amesema:

“Ibn Hazm amesema: “Bi maana ikisihi kwa mtazamo wake au kwa mtazamo wa imamu mwingine.”

Maneno yake yanayofuatia ni sahihi. an-Nawawiy (Rahimahu Allaah) amesema kwa kifupi:

“Watu wetu wameyatendea kazi haya inapokuja katika adhaana mbili, kushurutisha kutoka katika Ihraam kwa sababu ya maradhi na mengineyo ambayo yanatambulika katika vitabu vya madhehebu. Miongoni mwa watu ambao inasemekana wamefutu kutokana na Hadiyth ni Abu Ya´quub al-Buwaytiy na Abul-Qaasim ad-Daarikiy. Miongoni mwa waliyoyatendea kazi katika watu wetu Muhaddithun ni Imaam Abu Bakr al-Bayhaqiy na wengineo. Pindi baadhi ya marafiki zetu waliotangulia walipokuwa wanakutana na Hadiyth inayoenda kinyume na maoni ya ash-Shaafi´iy, basi wanaitendea kazi Hadiyth hiyo, wanafutu kwayo na wanasema:

“Madhehebu ya ash-Shaafi´iy ni yale yenye kuafikiana na Hadiyth.”

Shaykh Abu ´Amr amesema:

“Wale Shaafi´iyyah wanaopata Hadiyth inayoenda kinyume na madhehebu yake; ikiwa anakamilisha Ijtihaad kikamilifu (au katika mlango fulani au katika masuala fulani) basi aitendee kazi peke yake. Ikiwa hakukamilisha [sharti za Jihaad kikamilifu] na wakati huohuo anaona uzito kwenda kinyume na Hadiyth, aitendee kazi ikiwa kuna imaam mwingine mbali na ash-Shaafi´iy ambaye pekee yake aliitendea kazi. Hapa atakuwa na udhuru wa kuyaacha madhehebu ya imamu wake. Haya ambayo amesema ni mazuri na ni wajibu na Allaah ndiye anajua zaidi.”

Kuna sura nyingine ambayo Ibn-us-Swalaah hakuitaja; mtu afanye nini ikiwa hakupata mtu ambaye aliitendea kazi Hadiyth hiyo? Taqiyy-ud-Diyn as-Subkiy amejibu swali hili kwa kusema:

“Kwangu naona bora ni kufuata Hadiyth. Ajiweke nafasi ya kwamba yeye amemsikia Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) moja kwa moja kutoka kwake; hivi kweli inawezekana akachelewa kuitendea kazi? Ninaapa kwa Allaah, hapana! Kila mmoja ni mwenye kukalifishwa kwa mujibu wa uelewa wake.”  (Ma´naa Qawl-ish-Shaafi´iy ‘Idhaa swahh-al-Hadiyth’ (3/102))

Ukamilifu na uhakiki wa maudhui haya utayapata katika ”I´laam-ul-Muwaqqi´iyn” (2/202) na (2/370) na kitabu cha al-Fulaaniy kwa jina ”Iyqaadhw Himam Ulil-Abswaar”. Ni kitabu kizuri. Ni wajibu kwa kila ambaye anaipenda haki kukisoma kwa umakini.

[7] Hapa anayeambiwa ni Imaam Ahmad bin Hanbal (Rahimahu Allaah). Ameipokea Ibn Abiy Haatim katika ”Aadaab-ush-Shaafi´iy”, uk. 94-95, Abu Nu´aym katika ”al-Hilyah” (9/106), al-Khatwiyb katika ”al-Ihtijaaj bish-Shaafi´iy” (1/8) na kupitia kwake Ibn ´Asaakir (1/9/15), Ibn ´Abdil-Barr katika ”al-Intiqaa’”, uk. 75, Ibn-ul-Jawziy katika ”Manaaqib-ul-Imaam Ahmad”, uk. 499, na al-Harawiy (2/47/2) kupitia njia tatu kutoka kwa ´Abdullaah bin Ahmad bin Hanbal, kutoka kwa baba yake. Upokezi huo ni Swahiyh na ndio maana Ibn-ul-Jawziy ameutaja kwa njia ya kukata katika ”al-I´laam” (2/325) na al-Fulaaniy katika ”al-Iyqaadhw”, uk. 152, ambaye amesema:

“al-Bayhaqiy amesema: “Kwa ajili imekithiri kwake (yaani ash-Shaafi´iy) kuzichukua Hadiyth. Alikusanya elimu ya watu wa Hijaaz, Shaam na ´Iraaq na akachukua yale yote yaliyoshi kwa mtazamo wake pasi na kufadhilisha au kuegemea yale maoni ya watu wa nchi hiyo.”

[8] Abu Nu´aym katika ”al-Hilyah” (9/107), al-Harawiy (1/47), Ibn-ul-Qayyim katika ”I´laam-ul-Muwaqqi´iyn” (2/363) na al-Fulaaniy, uk. 104.

[9] Ibn Abiy Haatim katika ”Aadaab-ush-Shaafi´iy”, uk. 93, Abul-Qaasim as-Samarqandiy katika ”al-Amaaliy”, kama ilivyotajwa katika ”al-Muntaqaa” (1/234) cha Abu Hafsw al-Mu’adhdhin, Abu Nu´aym katika ”al-Hilyah” (9/106) na Ibn ´Asaakir (1/10/15) kwa cheni ya wapokezi Swahiyh.

[10] Ibn Abiy Haatim, uk. 93, Abu Nu´aym na Ibn ´Asaakir (2/9/15) kwa cheni ya wapokezi Swahiyh.

[11] Ibn Abiy Haatim, uk. 93-94.

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Swifatu Swalaat-in-Nabiy, uk. 44-47
  • Imechapishwa: 17/01/2019