07. Maamrisho ya Maalik ya kushikamana na Sunnah

2- Maalik bin Anas (Rahimahu Allaah)

Imaam Maalik bin Anas (Rahimahu Allaah) amesema:

1- “Hakika si vyengine mimi ni mtu ambaye mara hukosea na mara hupatia. Yatazame maoni yangu. Kila chenye kuafikiana na Qur-aan na Sunnah basi kichukue na kila ambacho hakiafikiani na Qur-aan na Sunnah achana nacho.”[1]

2- “Hakuna yeyote baada ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) isipokuwa maoni yake ima yanachukuliwa au yanarudishwa. Isipokuwa tu Mtume  (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).”[2]

3- Ibn Wahb amesema:

“Nilimsikia Maalik akiulizwa juu ya kuvichanganua vidole vya miguu wakati wa kutawadha. Akasema: “Haiwalazimu watu.” Sikusema kitu mpaka watu walipotawanyika. Nikamwambia: “Tuko na dalili juu ya hilo.” Akasema: “Ni ipi?” al-Layth bin Sa´d ametuhadithia, Ibn Lahiy´ah na ´Amr bin al-Haarith ametuhadithia, kutoka kwa Yaziyd bin ´Amr al-Ma´aafiriy, kutoka kwa Abiy ´Abdir-Rahmaan al-Hubuliy, kutoka kwa al-Mustawrid bin Shaddaad al-Qurashiy ambaye amesema:

“Nilimuona Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akisugua kati ya vidole vyake vya miguu kwa kidole chake kidogo.”

Akasema: “Hadiyth hii ni nzuri. Sijawahi kuisikia isipokuwa hivi sasa.” Kisha baada ya hapo nikamsikia anaulizwa kuhusu jambo hilo na akaamrisha kusugua baina ya vidole.”[3]

[1] Ibn ´Abdil-Barr katika ”al-Jaamiy´” (2/32) na kupitia kwake Ibn Hazm katika ”Usuul-ul-Ahkaam” (6/149) na al-Fulaaniy, uk. 72.

[2] Nukuu hii kutoka kwa Maalik imetangaa kwa wanachuoni waliokuja nyuma. Ibn ´Abdil-Haadiy ameisahihisha katika “Irshaad-us-Saalik” (1/227). Ibn ´Abdil-Barr ameipokea katika al-Jaamiy´” (2/91) na Ibn Hazm katika ”Usuul-ul-Ahkaam” (6/145) kutoka kwa al-Hakam bin ´Utaybah na Mujaahid. Taqiyy-ud-Diyn as-Subkiy ameitaja katika ”al-Fataawaa” (1/148) kutoka kwa Ibn ´Abbaas. Akapendekezwa na uzuri wake kisha akasema:

“Maneno haya ya Ibn ´Abbaas akayachukua Mujaahid na baadaye Maalik (Radhiya Allaahu ´anh) akayachukua kutoka kwao wawili. Yeye ndiye ametangaa kwayo.”

Halafu yakachukuliwa na Imaam Ahmad. Abu Daawuud amesema:

“Nilimsikia Ahmad akisema: “Hakuna yeyote baada ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) isipokuwa maoni yake ima yanachukuliwa au yanarudishwa.” (Masaa-il-ul-Imaam Ahmad, uk. 276)

[3] Ibn Abiy Haatim katika dibaji ya ”al-Jarh wat-Ta´diyl”, uk. 31-32. al-Bayhaqiy ameipokea katika ”as-Sunan” (1/81) kwa ukamilifu.

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Swifatu Swalaat-in-Nabiy, uk. 43-44
  • Imechapishwa: 17/01/2019