08. Je, inafaa kwa mwanamke kutoka kwenda sokoni pasi na kuwa na Mahram? Ni lini inafaa na lini inakuwa haramu?

Swali 08: Je, inafaa kwa mwanamke kutoka kwenda sokoni pasi na kuwa na Mahram? Ni lini inafaa na lini inakuwa haramu?

Jibu: Kimsingi ni kuwa inafaa kwa mwanamke kutoka kwenda sokoni. Si sharti awe na Mahram isipokuwa pale atapochelea fitina. Katika hali hiyo itamlazimu akitoka awe na Mahram wa kumlinda na kumuhifadhi. Ni sharti ili ifae kwake kutoka kwenda sokoni, atoke akiwa si mwenye kuonyesha mapambo na wala mwenye kujitia manukato. Akitoka hali ya kuwa ni mwenye kuonyesha mapambo au mwenye kujitia manukato, itakuwa si haramu kwake. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Msiwazuie wajakazi wa Allaah kutokamana na misikiti ya Allaah na watoke pasi na manukato wala kuonyesha mapambo.”[1]

Jengine ni kwa sababu kutoka kwao hali ya kuonyesha mapambo au kujitia manukato, kunatokea fitina kupitia wao na kutoka kwao. Kukiaminika fitina na mwanamke akatoka kwa njia inayotakikana – pasi na kuonyesha mapambo wala kujitia manukato – basi kutakuwa hakuna ubaya kwake kutoka. Wanawake katika zama za Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) walikuwa wakitoka kwenda katika masoko pasi na kuwa na Mahram.

[1] Ahmad na Abu Daawuud.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: As-ilah Muhimmah, uk. 15
  • Imechapishwa: 26/02/2023