Imaam ´Abdul-Ghaniy bin ´Abdil-Waahid al-Maqdisiy (Rahimahu Allaah) amesema:

201 – ´Abdullaah bin ´Umar (Radhiya Allaahu ´anhumaa) amesema:

“Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amekataza kuunganisha swawm. Wakasema: “Ee Mtume wa Allaah! Hakika wewe unafunga kwa kuunganisha.” Akasema: “Mimi si kama nyinyi. Mimi hulala nikilishwa na kunyweshwa na Mola wangu.”[1]

Ameipokea pia Abu Hurayrah, ´Aaishah na Anas bin Maalik (Radhiya Allaahu ´anhum).

202 – Muslim amepokea kupitia kwa Abu Sa´iyd al-Khudriy (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye amesema:

“Yeyote anayetaka kuunganisha basi aunganishe mpaka muda wa kabla kuingia alfajiri.”[2]

MAELEZO

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amekataza kuunganisha. Kuunganisha swawm (الوصال) maana yake ni mtu kuunganisha siku mbili au zaidi pamoja na nyusiku zake pasi na kula, kunywa wala kifunguzi kingine. Huku ndio kuunganisha ambapo mtu anaunganisha mchana na usiku vyote viwili na wala hali chochote; si usiku wala mchana, wala hanywi, wala hafanyi chochote katika vinavyofunguza. Hii ndio huitwa kuunganisha. Ameunganisha siku baada ya nyingine na amefanya usiku kama mchana ambapo hali ndani yake. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amewakataza kuunganisha kwa sababu ndani yake kuna uzito na ugumu. Allaah amewawekea Shari´ah Ummah yale mambo ambayo ndani yake kuna kuwafanyia wema, kuwahurumia na kuwafanyia upole. Hiyo ni fadhilah na wema kutoka kwa Allaah. Amesema (´Azza wa Jall):

يُرِيدُ اللَّـهُ بِكُمُ الْيُسْرَ وَلَا يُرِيدُ بِكُمُ الْعُسْرَ

“Allaah anakutakieni mepesi na wala hakutakieni mazito.”[3]

Allaah anarahisisha. Ndipo akawakataza kuunganisha kutokana na ule ugumu unaopatikana ndani yake. Wakasema: “Ee Mtume wa Allaah! Hakika wewe unafunga kwa kuunganisha.” Akasema:

“Mimi si kama nyinyi. Mimi hulala nikilishwa na kunyweshwa na Mola wangu.”

Imekuja katika tamko lingine:

“Mimi si mfano wenu.”

Imekuja katika tamko lingine:

“Mimi nina mwenye kuninywesha na mwenye kuninywesha.”[4]

Imekuja katika tamko lingine:

“Mimi hupata kivuli kwa Mola wangu ananilisha na kuninywesha.”[5]

Namna hii ndivo zilivyopokelewa Hadiyth kutoka kwa Ibn ´Umar, Abu Hurayrah, ´Aaishah, Anas na wengineo (Radhiya Allaahu ´anhum) zinazokataza kuunganisha. Katika upokezi wa Abu Sa´iyd uliopokelewa na Muslim imekuja:

“Yeyote anayetaka kuunganisha basi aunganishe mpaka wakati wakati wa mwisho wa usiku.”

[1] al-Bukhaariy (1962) na Muslim (1102).

[2] al-Bukhaariy (1963).

[3] 02:185

[4] al-Bukhaariy (1961, 1962, 1963, 1964, 1967) na Muslim (1102, 1110, 1103, 1104, 1105).

[5] Ahmad (8902), Khuzaymah (2072) na at-Twabaraaniy (5539).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Ifhaam fiy Sharh ´Umdat-il-Ahkaam (01/412-415)
  • Imechapishwa: 24/03/2022