Inatambulika pia kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alilingania katika dini ya Allaah na akatekeleza amri ya Allaah Makkah kwa kiasi cha uwezo wake. Vivyo hivyo Maswahabah (Radhiya Allaahu ´anhum) walifanya hivo kwa kiasi cha uwezo wao. Baadaye alipohama alitekeleza jambo la ulinganizi zaidi na kikamilifu zaidi. Wakati walipotawanyika katika miji baada ya kufa kwake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) walisimamia kazi hiyo (Radhiya Allaahu ´anhum). Kila mmoja alifanya kiasi cha uwezo na elimu yake. Kipindi ambacho walinganizi ni wachache, maovu ni mengi na kutandaa kwa ujinga – kama ilivyo hii leo – jambo la ulinganizi linakuwa ni faradhi kwa kila mmoja kwa kiasi cha uwezo wake. Ikiwa ni sehemu yenye ukomo, kama vile kijiji, mji na mfano wake na wakapatikana ambao watasimamia kazi hii na wakaisimamia kweli na kufikisha ujumbe wa Allaah, basi itatosha. Katika hali hiyo ufikishaji kwa wengine itakuwa ni jambo lenye kupendeza. Kwa sababu hoja itakuwa imesimama kupitia wengine na imetekelezeka amri ya Allaah kupitia mikono ya wengine. Kuhusu sehemu nyingine ya ardhi iliyosalia na watu wengine ni lazima kwa wanazuoni na watawala kwa kiasi cha uwezo wao wafikishe amri ya Allaah kwa kila njia wanayoiweza, jambo ambalo ni faradhi kwao kwa kiasi cha nguvu na uwezo wao.

Hivyo imejulikana kwamba kusema kuwa ni faradhi kwa kila mmoja na kuwa ni faradhi kwa baadhi ya watu ni jambo linategemea. Kulingania kunaweza kuwa ni faradhi kwa watu wote kwa nisba ya watu fulani kama ambavo inaweza kuwa ni jambo linalopendeza kwa nisba ya watu wengine. Kwa sababu kumepatikana nafasi na mahali pao ambao wamesimamia kazi hiyo na wakawatosheleza kutokamana nao.

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ad-Da´wah ilaa Allaah wa Akhlaaq-id-Du´aah, uk. 17-18
  • Imechapishwa: 31/05/2023