07. Mara faradhi kwa watu wote na mara nyingine faradhi kwa baadhi ya watu

Kwa hivyo ni lazima kwa wanazuoni, waumini na warithi wa Mitume kusimamia jukumu hili, wasaidiane na wawafikishie waja ujumbe wa Allaah na wasiogope kwa ajili ya Allaah lawama za mwenye kulaumu na wala wasimpendelei katika jambo hilo mdogo wala mkubwa, tajiri wala masikini. Bali wafikishe amri ya Allaah kwa waja wa Allaah kama alivyoteremshaAllaah na kama alivyosunisha Allaah. Pengine jambo hilo likawa ni faradhi kwa kila mmoja pale ambapo mtu atakuwa mahali ambapo hakuna mwingine awezaye kufanya kazi hiyo zaidi yako kama vile kuamrisha mema na kukataza maovu. Wakati fulani inakuwa ni faradhi kwa kila mmoja na wakati mwingine inakuwa ni faradhi kwa baadhi ya watu. Unapokuwa sehemu ambayo hakuna mwingine awezaye kusimamia kazi hii na akafikisha amri ya Allaah zaidi yako, basi itakulazimu kusimamia kazi hiyo. Lakini kukipatikana wengine ambao wanasimamia kazi ya kulingania, kufikisha, kuamrisha na kukataza, basi hapo juu yako itakuwa ni jambo linalopendeza. Ukikimbilia na kupupia jambo hilo basi utakuwa wakati huo ni mwenye kushindana katika mambo ya kheri na mwenye kutangulia katika matendo mema. Miongoni mwa dalili zilizotumiwa ya kwamba ni faradhi kwa baadhi ya watu ni maneno Yake (´Azza wa Jall):

وَلْتَكُن مِّنكُمْ أُمَّةٌ يَدْعُونَ إِلَى الْخَيْرِ

“Wawepo kutoka kwenu watu wanaolingania kheri.”[1]

Haafidhw Ibn Kathiyr amesema katika mnasaba wa Aayah hii maneno yenye maana isemayo:

“Kuweko miongoni mwenukikundi kinachosimamia jukumu hili kubwa; kinalingania kwa Allaah, kinaeneza dini Yake na kinafikisha jambo Lake (Subhaanahu wa Ta´ala).”

[1] 03:104

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ad-Da´wah ilaa Allaah wa Akhlaaq-id-Du´aah, uk. 16-17
  • Imechapishwa: 31/05/2023