08. ´Arshiy iko juu ya maji na Allaah yuko juu ya ´Arshiy

Allaah ameziumba mbingu saba baadhi juu ya nyingine na ardhi saba baadhi chini ya nyingine. Baina ya ardhi ya juu kabisa na mbingu ya chini kabisa kuna mafasa ya miaka 500. Masafa ya kila mbingu ni miaka 500.

Maji yako juu ya mbingu ya saba na ya juu kabisa. ´Arshi ya Mwingi wa huruma (´Azza wa Jall) iko juu ya maji na Allaah (´Azza wa Jall) yuko juu ya ´Arshi.

al-Kursiy ni mahali pa kuwekea miguu.

Anayajua yaliyomo ndani ya mbingu na ardhi saba, yaliyoko baina yavyo na yaliyoko chini ya udongo, katika shina ya bahari, kumea kwa kila unywele, kila mti, kila mmea, kila jani lililoanguka na idadi yake. Anadhibiti hesabu ya kokoto zote, uzito wa milima yote na matone ya mvua, matendo yote yanayofanywa na waja na athari wanazoacha na kusema, pumzi zao, manung´uniko yao na yale yanayowazwa na vifua vyao. Anakijua kila kitu. Hakuna chochote katika hayo kinachojificha Kwake.

Yuko juu ya ´Arshi juu ya mbingu ya saba. Amekingwa na pazia ya moto, nuru, giza na mengine Anayoyajua Yeye pekee.

Ikiwa mzushi, mpinzani au zandiki atajengea hoja maneno Yake Allaah (Tabaarak wa Ta´ala):

وَلَقَدْ خَلَقْنَا الْإِنسَانَ وَنَعْلَمُ مَا تُوَسْوِسُ بِهِ نَفْسُهُ ۖ وَنَحْنُ أَقْرَبُ إِلَيْهِ مِنْ حَبْلِ الْوَرِيدِ

“Hakika Tumemuumba mwanaadamu na tunajua yale  yanayomshawishi nafsi yake na Sisi tuko karibu naye kuliko mshipa wa shingo.”[1]

هُوَ الَّذِي خَلَقَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ فِي سِتَّةِ أَيَّامٍ ثُمَّ اسْتَوَى عَلَى الْعَرْشِ يَعْلَمُ مَا يَلِجُ فِي الْأَرْضِ وَمَا يَخْرُجُ مِنْهَا وَمَا يَنزِلُ مِنَ السَّمَاء وَمَا يَعْرُجُ فِيهَا وَهُوَ مَعَكُمْ أَيْنَ مَا كُنتُمْ ٌ

”Yeye Ndiye Aliyeumba mbingu na ardhi katika siku sita, kisha Akalingana juu ya ´Arshi. Anajua yanayoingia ardhini, na yatokayo humo, na yanayoteremka kutoka mbinguni, na yanayopanda humo. Naye Yu Pamoja nanyi popote mlipo.”[2]

أَلَمْ تَرَ أَنَّ اللَّـهَ يَعْلَمُ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَمَا فِي الْأَرْضِ ۖ مَا يَكُونُ مِن نَّجْوَىٰ ثَلَاثَةٍ إِلَّا هُوَ رَابِعُهُمْ وَلَا خَمْسَةٍ إِلَّا هُوَ سَادِسُهُمْ وَلَا أَدْنَىٰ مِن ذَٰلِكَ وَلَا أَكْثَرَ إِلَّا هُوَ مَعَهُمْ أَيْنَ مَا كَانُوا

“Je, huoni kwamba Allaah Anajua yale yote yaliyomo mbinguni na yale yote yaliyomo ardhini? Hauwi mnong’ono wa watatu isipokuwa Yeye ni wa nne wao, na wala watano isipokuwa Yeye ni wa sita wao, na wala [hauwi mnong’ono wa] chini kuliko ya hivyo, na wala wa wengi zaidi isipokuwa Yeye Yu pamoja nao popote watakapokuwa.”[3]

na Aayah nyingine ambazo haziko wazi, basi mwambie kuwa Anachokusudia ni utambuzi. Allaah (Ta´ala) yuko juu ya ´Arshi juu ya mbingu ya saba ilioko juu kabisa na anakijua kila kitu. Ametengana kutokamana na viumbe Wake ilihali utambuzi Wake uko kila mahali.

Allaah (´Azza wa Jall) anayo ´Arshi na ´Arshi iko na wabebaji wanaoibeba.

Ana mpaka na Allaah ndiye mtambuzi zaidi wa mpaka Wake.

Allaah yuko juu ya ´Arshi na hakuna mungu wa haki mwingine asiyekuwa Yeye.

[1] 50:16

[2] 57:4

[3] 58:7

  • Mhusika: Imaam Harb bin Ismaa´iyl al-Kirmaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Kitaab-us-Sunnah, uk. 54-59
  • Imechapishwa: 25/05/2022