Kuhusu kuamini Qadar kheri na shari yake, inahusiana na kuthibitisha kwa kukata kabisa ya kwamba Allaah alikadiria makadirio ya viumbe na kwamba yale yote yaliyopitika, Allaah aliyataka, na yale yote ambayo hayakupitika, Allaah hakuyataka. Allaah (Ta´ala) amesema:

إِنَّا كُلَّ شَيْءٍ خَلَقْنَاهُ بِقَدَرٍ

“Hakika sisi tumekiumba kila kitu kwa makadirio.” (54:49)

وَكَانَ أَمْرُ اللَّـهِ قَدَرًا مَّقْدُورًا

“Na amri ya Allaah daima ni makadirio yaliyokadiriwa.” (33:38)

Qadar ina daraja nne:

1- Tunaamini kuwa Allaah (Ta´ala) anakijua kila kitu. Anakijua kila kilichokuwepo, kilichopo na vipi kitakuwa kwa elimu Yake ya milele. Hajiwi na elimu mpya baada ya kutokujua na wala hasahau baada ya kujua.

2- Tunaamini kuwa Allaah aliandika katika Ubao uliohifadhiwa kila kitachokuwepo mpaka Qiyaamah kisimame. Amesema (Ta´ala):

أَلَمْ تَعْلَمْ أَنَّ اللَّـهَ يَعْلَمُ مَا فِي السَّمَاءِ وَالْأَرْضِ ۗ إِنَّ ذَٰلِكَ فِي كِتَابٍ ۚ إِنَّ ذَٰلِكَ عَلَى اللَّـهِ يَسِيرٌ

“Je, hujui kwamba Allaah anajua yale yote yaliyomo katika mbingu na ardhi? Hakika hayo yamo katika Kitabu. Hakika hayo kwa Allaah ni mepesi.” (22:70)

قَالَ فَمَا بَالُ الْقُرُونِ الْأُولَىٰ قَالَ عِلْمُهَا عِندَ رَبِّي فِي كِتَابٍ ۖ لَّا يَضِلُّ رَبِّي وَلَا يَنسَى

“Akasema: “Basi nini hali ya karne za  mwanzoni?” Akasema: “Ujuzi wake uko kwa Mola wangu katika Kitabu. Hapotezi Mola wangu na wala hasahau.” (20:51-52)

وَكُلَّ شَيْءٍ أَحْصَيْنَاهُ فِي إِمَامٍ مُّبِينٍ

“Kila kitu Tumekirekodi barabara katika kitabu kinachobainisha.” (36:12)

Katika nukta hii kunaingia vilevile makadirio ya milele kabla ya kuumba mbingu na ardhi. Amesema (Ta´ala):

قُل لَّن يُصِيبَنَا إِلَّا مَا كَتَبَ اللَّـهُ لَنَا

“Sema: “Halitusibu lolote isipokuwa lile alilotukidhia Allaah.” (09:51)

Kadhalika inahusiana na Siku makubaliano yalipoandikwa:

أَلَسْتُ بِرَبِّكُمْ

“Je, Mimi siye Mola wenu?” (07:172)

Amesema (Ta´ala):

وَإِذْ أَخَذَ رَبُّكَ مِن بَنِي آدَمَ مِن ظُهُورِهِمْ ذُرِّيَّتَهُمْ وَأَشْهَدَهُمْ عَلَىٰ أَنفُسِهِمْ أَلَسْتُ بِرَبِّكُمْ ۖقَالُوا بَلَىٰ

“Na pindi Mola wako alipochukua katika wana wa Aadam kutoka migongoni mwao kizazi chao na akawashuhudisha juu ya nafsi zao: “Je, Mimi siye Mola wenu?” Wakasema: “Ndiye.” (07:172)

Kuhusu makadirio ya kiumri, yanapitika pale tone la mbegu linapotumbukia kwenye kifuko cha uzazi. Ndipo hutumwa Malaika anayepulizia kipande cha nyama roho na anaamrishwa mambo mane; riziki yake, muda atakaoeshi, matendo yake na kama atakuwa mwenye furaha au mla hasara.

Ama kuhusu makadirio ya mwaka, yanapitika katika usiku wenye Cheo. Amesema (Ta´ala):

فِيهَا يُفْرَقُ كُلُّ أَمْرٍ حَكِيمٍ

“Humo hupambanuliwa kila jambo la hekima.” (44:04)

Ibn ´Abbaas amesema:

“Katika usiku wenye Cheo kunaandikwa kwenye mama wa Kitabu yatayokuwepo katika mwaka katika kifo, uhai, riziki, mvua na mahujaji. Kunasemwa: “Atahiji fulani, atahiji fulani.””

Kuhusu makadirio ya kila siku, amesema (Ta´ala):

كُلَّ يَوْمٍ هُوَ فِي شَأْنٍ

“Kila siku Yeye yumo katika kuleta jambo.” (55:29)

Makadirio ya kila siku ni upambanuzi wa makadirio ya mwaka, makadirio ya mwaka ni upambanuzi wa makadirio ya umri pindi linapoumbwa tone la manii, makadirio ya umri ni upambanuzi wa makadirio ya umri ya mwanzo pindi ilipopitika Siku ya makubaliano ambapo pia ni upambanuzi wa makadirio ya milele ambayo Kalamu iliandika kwenye Kitabu kinachobainisha. Kitabu hichi chenye kubainisha ni katika elimu ya Allaah (´Azza wa Jall). Kadhalika kikomo cha makadirio kinaishia katika elimu ya Allaah (´Azza wa Jall):

وَأَنَّ إِلَىٰ رَبِّكَ الْمُنتَهَىٰ

“Na kwamba kwa Mola wako ndio kikomo.” (53:42)

3- Utashi. Tunaamini kuwa Allaah (Ta´ala) ametaka kila kilichomo mbinguni na ardhini. Hakukuwi kitu isipokuwa kwa kutaka Kwake. Anachokitaka, huwa, na asichokitaka, hakiwi. Amesema (Ta´ala):

إِنَّمَا أَمْرُهُ إِذَا أَرَادَ شَيْئًا أَن يَقُولَ لَهُ كُن فَيَكُونُ

“Hakika amri Yake anapotaka chochote hukiambia: “Kuwa!” – nacho huwa.” (36:82)

وَلَوْ شَاءَ اللَّـهُ مَا اقْتَتَلُوا

“Na lau angelitaka Allaah wasingelipigana.” (02:253)

وَلَوْ شَاءَ اللَّـهُ لَجَمَعَهُمْ عَلَى الْهُدَىٰ

“Na kama angetaka Allaah basi angeliwakusanya katika uongofu.” (06:35)

وَلَوْ شَاءَ رَبُّكَ لَجَعَلَ النَّاسَ أُمَّةً وَاحِدَةً

“Na kama angetaka Mola wako, basi angejaalia watu wote kuwa ni ummah mmoja.” (11:118)

وَلَوْ شِئْنَا لَآتَيْنَا كُلَّ نَفْسٍ هُدَاهَا وَلَـٰكِنْ حَقَّ الْقَوْلُ مِنِّي

“Na Tungelitaka, basi tungeliipa kila nafsi mwongozo wake, lakini imethibiti kauli kutoka Kwangu.” (32:13)

وَمَا كَانَ اللَّـهُ لِيُعْجِزَهُ مِن شَيْءٍ فِي السَّمَاوَاتِ وَلَا فِي الْأَرْضِ

“Na hakuna lolote limshindalo Allaah mbinguni na wala ardhini.” (35:44)

4- Uumbaji. Hakika Yeye (Ta´ala) ndiye ameumba kila mtendaji na matendo yake, kila mwenye kutikisika na kutikisika kwake na kila mwenye kutulia na kutulia kwake. Amesema (Ta´ala):

وَاللَّـهُ خَلَقَكُمْ وَمَا تَعْمَلُونَ

“Allaah amekuumbeni na yale mnayoyatenda.” (37:96)

اللَّـهُ خَالِقُ كُلِّ شَيْءٍ ۖ وَهُوَ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ وَكِيلٌ

“Allaah ni Muumbaji wa kila kitu, Naye juu ya kila kitu ni mdhamini anayetegemewa kwa yote.” (39:62)

Pamoja na hivyo tunaamini kuwa waja wana uwezo, utashi na matakwa juu ya matendo yao. Allaah (Ta´ala) ndiye amewaumba wao na matakwa yao, uwezo wao, maneno yao na matendo yao. Maneno na vitendo vinavyotoka kwao, vinanasibishwa kwao kihakika na kwavyo ndivyo ima watalipwa thawabu au adhabu. Hata hivyo wao hawawezi isipokuwa yale ambayo Allaah (Ta´ala) amewawezesha na wala hawatotaka isipokuwa Allaah akitaka kwanza. Amesema (Ta´ala):

إِنَّ هَـٰذِهِ تَذْكِرَةٌ ۖ فَمَن شَاءَ اتَّخَذَ إِلَىٰ رَبِّهِ سَبِيلًا وَمَا تَشَاءُونَ إِلَّا أَن يَشَاءَ اللَّـهُ ۚ إِنَّ اللَّـهَ كَانَ عَلِيمًا حَكِيمًا

“Hakika huu ni ukumbusho, basi anayetaka achukue njia ya Mola wake. Na hamtoweza kutaka chochote isipokuwa atake Allaah – hakika Allaah daima ni Mjuzi wa yote, Mwenye hekima.” (76:29-30)

إِنْ هُوَ إِلَّا ذِكْرٌ لِّلْعَالَمِينَ لِمَن شَاء مِنكُمْ أَن يَسْتَقِيمَ وَمَا تَشَاؤُونَ إِلَّا أَن يَشَاء اللَّهُ رَبُّ الْعَالَمِينَ

“Haikuwa huu isipokuwa ni Ukumbusho kwa walimwengu wote – kwa yule miongoni mwenu anayetaka anyooke. Wala nyinyi hamtataka isipokuwa atake Allaah, Mola wa walimwengu.” (81:27-29)

لَا يُكَلِّفُ اللَّـهُ نَفْسًا إِلَّا وُسْعَهَا ۚ لَهَا مَا كَسَبَتْ وَعَلَيْهَا مَا اكْتَسَبَتْ

“Allaah hakalifishi nafsi yoyote isipokuwa kwa kadiri ya uwezo wake. Itapata [thawabu] iliyoyachuma na ni dhidi yake [kwa dhambi] iliyojichumia.” (02:286)

وَتِلْكَ الْجَنَّةُ الَّتِي أُورِثْتُمُوهَا بِمَا كُنتُمْ تَعْمَلُونَ

“Na hiyo ni Pepo ambayo mmerithishwa kwa yale mliyokuwa mkitenda.” (43:72)

Bi maana kwa sababu ya matendo. Vilevile amesema (Ta´ala):

وَذُوقُوا عَذَابَ الْخُلْدِ بِمَا كُنتُمْ تَعْمَلُونَ

“Onjeni adhabu yenye kudumu kwa yale mliyokuwa mkiyatenda.” (32:14)

فَمَن يَعْمَلْ مِثْقَالَ ذَرَّةٍ خَيْرًا يَرَهُ وَمَن يَعْمَلْ مِثْقَالَ ذَرَّةٍ شَرًّا يَرَهُ

“Basi yule atakayetenda kheri sawa na uzito wa chembe ya atomu, basi ataiona, na yule atakayetenda shari sawa na uzito wa chembe ya atomu, basi ataiona.” (99:07-08)

Tunaamini kuwa makadirio yaliyotangulia hayamzuii mtu na kutenda kama ambavyo vilevile hayamfanyi mtu kuacha kufanya matendo. Pindi Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipowaeleza Maswahabah zake juu ya Qadar, na kwamba yameanza kufanya kazi na kwamba kalamu imekauka, wakamwambia:

“Tusitegemee yaliyopangwa kwetu na tukaacha kutenda?”

Akasema:

“Hapana. Tendeni, kila kitu kimewepesishwa.”

Halafu akasoma:

فَأَمَّا مَنْ أَعْطَىٰ وَاتَّقَىٰ وَصَدَّقَ بِالْحُسْنَىٰ فَسَنُيَسِّرُهُ لِلْيُسْرَىٰ وَأَمَّا مَن بَخِلَ وَاسْتَغْنَىٰ وَكَذَّبَ بِالْحُسْنَىٰ فَسَنُيَسِّرُهُ لِلْعُسْرَىٰ

“Basi yule anayetoa na akamcha Allaah na akasadikisha lililo jema zaidi, basi tutamuwepesishia kwa yaliyo mepesi. Ama yule afanyaye ubakhili na akajiona amejitosheleza na akakadhibisha lililo jema zaidi, basi tutamuwepesishia kwa yaliyo magumu.” (92:05-10)

Makadirio yana sababu zinazomfanya mtu akayafikia. Kama ambavyo kuoa ni sababu inayopelekea kupata kizazi na kilimo ni sababu inayopelekea katika mavuno, kadhalika matendo mema ni sababu inayopelekea kuingia Peponi na matendo mabaya ni sababu inayopelekea katika Moto.

  • Mhusika: Shaykh ´Abdus-Salaam bin Barjas
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Mu´taqad as-Swahiyh, uk. 57-63
  • Imechapishwa: 21/06/2020