07. Waja Ramadhaan wametunukiwa kwa njia tatu kuu

Amewatunuku waja Wake (Subhaanah) kwa ujira huu kwa njia tatu zifuatazo:

1- Amewawekea katika Shari´ah matendo mema ambayo ni sababu ya kuwasamehe madhambi yao na kuzinyanyua daraja zao. Asingeliwawekea Shari´ah hiyo basi ingelikuwa haifai kwao kumwabudu kwazo. Kwani ´ibaadah haichukuliwi isipokuwa kutoka katika Wahy wa Allaah kwenda kwa Mitume Yake. Kwa ajili hiyo Allaah amewakaripia wale wenye kujiwekea mambo katika Shari´ah kutoka katika vichwa vyao na akafanya kitendo hicho ni aina fulani ya shirki. Amesema (Subhaanah):

أَمْ لَهُمْ شُرَكَاءُ شَرَعُوا لَهُم مِّنَ الدِّينِ مَا لَمْ يَأْذَن بِهِ اللَّـهُ

“Je, wanao washirika wanaowatungia Shari´ah yale ambayo Allaah hakuyaidhinisha?”[1]

2- Amewawafikisha kutenda matendo mema yaliyoachwa na watu wengi. Pasi na Allaah kuwasaidia na kuwawafikisha basi wasingeliyafanya. Fadhilah na neema ni za Allaah kwa mambo hayo:

يَمُنُّونَ عَلَيْكَ أَنْ أَسْلَمُوا ۖ قُل لَّا تَمُنُّوا عَلَيَّ إِسْلَامَكُم ۖ بَلِ اللَّـهُ يَمُنُّ عَلَيْكُمْ أَنْ هَدَاكُمْ لِلْإِيمَانِ إِن كُنتُمْ صَادِقِينَ

“Wanadhani wamekufanyia fadhilah kwamba wamesilimu? Sema: “Msidhani mmenifanyia fadhilah kusilimu kwenu. Bali Allaah ndiye amekufanyieni fadhilah kwa kukuongozeni katika imani mkiwa ni wakweli.”[2]

3- Amewatunuku kwa kheri nyingi ambapo tendo moja jema linalipwa kwa matendo kumi mfano wake mpaka mara mia saba na zaidi ya hapo. Fadhilah ni kutoka kwa Allaah kwa kutenda na kwa kumlipa thawabu mtu huyo na himdi zote zinamstahikia Allaah, Mola wa walimwengu.

[1] 42:21

[2] 49:71

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majaalis Shahr Ramadhwaan, uk. 10-11
  • Imechapishwa: 07/04/2020