Amesema (´Azza wa Jall):

وَاللَّـهُ خَلَقَكُم مِّن تُرَابٍ

”Allaah amekuumbeni kutokana na udongo.”[1]

Kisha akasema:

إِنَّا خَلَقْنَاهُم مِّن طِينٍ لَّازِبٍ

”… hakika Sisi tumewaumba kutokana na udongo unaonata.”[2]

Kisha akasema:

وَلَقَدْ خَلَقْنَا الْإِنسَانَ مِن صَلْصَالٍ مِّنْ حَمَإٍ مَّسْنُونٍ

”Na kwa hakika Tumemuumba mtu kutokana na udongo wa mfinyanzi unaotoa sauti, unaotokana na tope nyeusi iliyogeuka rangi na harufu yake.”[3]

Halafu akasema:

وَلَقَدْ خَلَقْنَا الْإِنسَانَ مِن سُلَالَةٍ مِّن طِينٍ

“Kwa hakika Tumemuumba mtu kutokana na mchujo safi wa udongo.”[4]

Kisha akasema:

خَلَقَ الْإِنسَانَ مِن صَلْصَالٍ كَالْفَخَّارِ

“Amemuumba mtu kutokana na udongo wa mfinyanzi unaotoa sauti kama wa vyungu uliookwa moto.”[5]

Wakaitilia shaka Qur-aan na kusema kuwa ni ubabaishaji unaogongana.

Bali hivo ndivo Allaah alivoanza kumuumba Aadam; Allaah alianza kumuumba kwa udongo, kisha kwa udongo mwekundu, mweusi na mweupe, kwa udongo wenye rutuba na udongo usio na rutuba. Vivyo hivyo kizazi chake wako walio wazuri na wabaya, weusi, wekundu na weupe. Baada ya hapo akautia maji udongo huo na ukawa ni udongo unaonata, udongo huo ukawa:

مِّن طِينٍ لَّازِبٍ

”… kutokana na udongo unaonata.”

Kisha akasema:

مِن سُلَالَةٍ مِّن طِينٍ

”… kutokana na mchujo safi wa udongo.”

Udongo huo unakuwa namna hiyo wakati unapokandamizwa na kukamuliwa unatoka kati ya vidole.

Kisha ukabaki hivo kitambo fulani na ukawa tope nyeusi iliyogeuka rangi na harufu yake. Akaumbwa kutokana na tope nyeusi iliyogeuka rangi na harufu yake. Lilipokauka, likawa ni udongo wa mfinyanzi unaotoa sauti, kama chombo cha udongo. Hapa kunabainishwa namna alivyoumbwa Aadam.

Kuhusu maneno Yake:

ثُمَّ جَعَلَ نَسْلَهُ مِن سُلَالَةٍ مِّن مَّاءٍ مَّهِينٍ

”… kisha akajaalia kizazi chake kutokana na mchujo safi wa maji dhalilifu.”[6]

kunakusudiwa mwanzo mwa kuumbwa kizazi chake na inatokana na shawaha inayotoka kwa mwanamme. Hiyo ndio maana ya:

مِّن مَّاءٍ مَّهِينٍ

”… kutokana na mchujo safi wa maji dhalilifu.”

Bi maana maji dhaifu. Haya ndio waliyotilia mashaka mazanadiki.

[1] 35:11

[2] 37:11

[3] 15:26

[4] 23:12

[5] 55:14

[6] 32:8

  • Mhusika: Imaam Ahmad bin Hanbal (afk. 241)
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ar-Radd ´alaal-Jahmiyyah waz-Zanaadiqah, uk. 66-68
  • Imechapishwa: 03/04/2024