07. Masuala matatu wajibu kuyatambua na kuyatendea kazi

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Tambua – Allaah Akurehemu – kwamba ni wajibu kwa kila Muislamu mwanaume na mwanamke, kujifunza masuala haya matatu na kuyatendea kazi:

La kwanza: Allaah Ametuumba, akaturuzuku na Hakutuacha bure tu bila ya malengo. Bali Amewatumia Mtume; mwenye kumtii, ataingia Peponi, na yule mwenye kumuasi, ataingia Motoni. Dalili ni Kauli Yake (Ta´ala):

إِنَّا أَرْسَلْنَا إِلَيْكُمْ رَسُولًا شَاهِدًا عَلَيْكُمْ كَمَا أَرْسَلْنَا إِلَىٰ فِرْعَوْنَ رَسُولًا فَعَصَىٰ فِرْعَوْنُ الرَّسُولَ فَأَخَذْنَاهُ أَخْذًا وَبِيلًا

“Hakika Sisi Tumekutumieni Mtume awe ni shahidi juu yenu, kama Tulivyotuma kwa Fir’awn Mtume. Lakini Fir’awn alimuasi huyo Mtume, Tukamuadhibu adhabu kali sana.” (al-Muzzammil 73 : 15-16)

La pili: Hakika Allaah Haridhii kushirikishwa pamoja Naye yeyote katika ´ibaadah Yake; si Malaika aliyekaribu wala Mtume aliyetumwa. Dalili ni Kauli Yake (Ta´ala):

وَأَنَّ الْمَسَاجِدَ لِلَّـهِ فَلَا تَدْعُوا مَعَ اللَّـهِ أَحَدًا

“Hakika Misikiti yote ni ya Allaah, basi msiombe [msimuabudu] yeyote pamoja na Allaah.” (al-Jinn 72 : 18)

La tatu: Mwenye kumtii Mtume na akampwekesha Allaah Mmoja, basi haijuzu kwake kufanya urafiki na wale wanaompinga Allaah na Mtume Wake, hata kama itakuwa ni jamaa wa karibu. Dalili ni Kauli Yake (Ta´ala):

لَّا تَجِدُ قَوْمًا يُؤْمِنُونَ بِاللَّـهِ وَالْيَوْمِ الْآخِرِ يُوَادُّونَ مَنْ حَادَّ اللَّـهَ وَرَسُولَهُ وَلَوْ كَانُوا آبَاءَهُمْ أَوْ أَبْنَاءَهُمْ أَوْ إِخْوَانَهُمْ أَوْ عَشِيرَتَهُمْ ۚ أُولَـٰئِكَ كَتَبَ فِي قُلُوبِهِمُ الْإِيمَانَ وَأَيَّدَهُم بِرُوحٍ مِّنْهُ

“Hutokuta watu wanaomuamini Allaah na Siku ya Mwisho kuwa wanawapenda wale wanaopinzana na Allaah na Mtume Wake, japo wakiwa ni baba zao, watoto wao, ndugu zao au jamaa zao. Hao [Allaah] Amewaandikia katika nyoyo zao imani na Akawatia nguvu kwa Roho kutoka Kwake, na Atawaingiza kwenye mabustani yapitayo chini yake mito, ni wenye kudumu humo. Allaah Ameridhika nao, nao wameridhika Naye. Hao ndio kundi la Allaah. Tanabahi! Hakika kundi la Allaah ndio lenye kufaulu.”
(al-Mujaadalah 58 : 22)

MAELEZO

Masuala matatu ni katika mambo muhimu yanayohusiana na Tawhiyd na haki za Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala).

Allaah amewaumba viumbe ili wamuabudu. Hakuwaumba bure wala pasi na malengo. Amewaumba kwa ajili ya jambo muhimu na kwa hekima kubwa. Humo ndio kuna furaha yao. Humo ndio kuna uokovu wao. Inahusu kumuabudu Allaah peke yake. Allaah (Ta´ala) amesema:

وَمَا خَلَقْتُ الْجِنَّ وَالْإِنسَ إِلَّا لِيَعْبُدُونِ

“Sikuumba majini na wanaadamu isipokuwa waniabudu.” (51:56)

´Ibaadah hii ndio Allaah kawaamrisha nayo aliposema:

يَا أَيُّهَا النَّاسُ اعْبُدُوا رَبَّكُمُ

“Enyi watu! Mwabuduni Mola wenu.” (02:21)

وَقَضَىٰ رَبُّكَ أَلَّا تَعْبُدُوا إِلَّا إِيَّاهُ

“Mola wako amehukumu kwamba: “Msiabudu yeyote isipokuwa Yeye pekee.”” 17:23

وَاعْبُدُوا اللَّـهَ وَلَا تُشْرِكُوا بِهِ شَيْئًا

“Mwabuduni Allaah na wala msimshirikishe Yeye na chochote.” (04:36)

فَاعْبُدِ اللَّـهَ مُخْلِصًا لَّهُ الدِّينَ

“Basi mwabudu Allaah pekee hali ya kumtakasia Yeye dini.” (39:02)

وَمَا أُمِرُوا إِلَّا لِيَعْبُدُوا اللَّـهَ مُخْلِصِينَ لَهُ الدِّينَ

“Hawakuamrishwa jengine isipokuwa wamuabudu Allaah kwa imani safi kabisa na ya asli hali ya kumtakasia Yeye dini.” (98:05)

Katika Aayah nyingi amewaamrisha wamuabudu Yeye pekee. Anatakiwa kukhusishwa kwa ´ibaadah kukiwemo du´aa, khofu, matarajio, kutegemea, shauku, woga, swalah na swawm. Yeye (Subhaanah) ndiye mwenye kustahiki kuabudiwa pasi na mwengine. Katika ´ibaadah kunaingia vilevile kutekeleza maamrisho na kujiepusha na makatazo. Kufanya maamrisho aliyoamrisha Allaah na Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni ´ibaadah. Kujiepusha na makatazo aliyokukataza Allaah na Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni ´ibaadah. Huu ndio Uislamu. Hii ndio dini. Hii ndio imani. Huu ndio uongofu.

Usiswali kwa ajili ya mwingine asiyekuwa Allaah. Usirukuu kwa ajili ya mwingine asiyekuwa Allaah. Usichinje kwa ajili ya mwingine asiyekuwa Allaah. Usimuombe mwingine asiyekuwa Allaah. Usimtegemee mwengine isipokuwa Yeye na mengineyo.

Hata hivyo kumtaka msaada ambaye yuko mbele yako na ni muweza sio ´ibaadah. Allaah (Subhaanah) amesema kuhusu Muusa:

فَاسْتَغَاثَهُ الَّذِي مِن شِيعَتِهِ عَلَى الَّذِي مِنْ عَدُوِّهِ

“Akamsaidia yule ambaye katika kundi lake dhidi ya yule ambaye ni katika adui wake.” (28:15)

Kwa kuwa Muusa alikuwa anaweza kumsaidia.

Kuhusu kuwaomba maiti, kuwaomba wasiokuwepo ambao hawasikii au sanamu, jini, mti na mfano wa hayo ndio shirki ya washirikina na ni shirki kubwa. Allaah (Ta´ala) amesema kuwa Luqmaan amesema kuhusu hilo:

يَا بُنَيَّ لَا تُشْرِكْ بِاللَّـهِ ۖ إِنَّ الشِّرْكَ لَظُلْمٌ عَظِيمٌ

“Ee mwanangu! Usimshirikishe Allaah; hakika shirki ni dhulma kubwa mno!” (31:13)

وَلَوْ أَشْرَكُوا لَحَبِطَ عَنْهُم مَّا كَانُوا يَعْمَلُونَ

“Lau wangemshirikisha bila shaka yangebatilika yale waliyokuwa wakitenda.” (6:88)

إِنَّ اللَّـهَ لَا يَغْفِرُ أَن يُشْرَكَ بِهِ وَيَغْفِرُ مَا دُونَ ذَٰلِكَ لِمَن يَشَاءُ

“Hakika Allaah hasamehi kushirikishwa na anasamehe yaliyo chini ya hayo kwa Amtakae.” (4:48)

وَلَقَدْ أُوحِيَ إِلَيْكَ وَإِلَى الَّذِينَ مِن قَبْلِكَ لَئِنْ أَشْرَكْتَ لَيَحْبَطَنَّ عَمَلُكَ وَلَتَكُونَنَّ مِنَ الْخَاسِرِينَ

“Hakika umefunuliwa Wahy wewe na kwa wale walio kabla yako kwamba ukishirikisha bila shaka yatabatilika matendo yako na utakuwa miongoni mwa waliokhasirika.” (39:65)

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 13-15
  • Imechapishwa: 15/10/2016