ash-Shaafi´iy[1] (Rahimahu Allaah) amesema:

“Lau Allaah Asingeliteremsha hoja yoyote kwa viumbe Wake isipokuwa Suurah hii, basi ingeliwatosheleza.”

Katika upokezi mwingine imekuja:

“Lau watu wangeliitafakari Suurah hii, basi ingeliwatosheleza.”

Bi maana lau wangeliitafakari na kuizingatia basi ingeliwatosheleza katika kushikamana na haki, kutekeleza maamrisho ya Allaah na kujiepusha na makatazo Yake. Allaah amebainisha kuwa wale walioamini, wakatenda matendo mema, wakausiana kwa haki na wakausiana kuwa na subira ndio wenye kufuzu na wengine wote wamekula khasara. Mlango huu unathibitisha kuwa ni wajibu kuusiana, kupeana nasaha, kuamini, kusubiri na kuwa na ukweli na kwamba hakuna njia ya kufikia furaha isipokuwa kwa mambo haya mane: kuwa na imani ya kweli kwa Allaah na Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), matendo mema, kuusiana juu ya haki na kuusiana juu ya subira.

al-Bukhaariy[2] (Rahimahu Allaah) amesema:

“Mlango: Elimu kabla ya kauli na kitendo. Dalili ni Kauli Yake (Ta´ala):

فَاعْلَمْ أَنَّهُ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا اللَّـهُ وَاسْتَغْفِرْ لِذَنبِكَ

“Basi elewa kwamba hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah na omba msamaha kwa dhambi zako.” (47:19)

Akawa ameanza kwa elimu kabla ya kauli na kitendo.”

Mtu anatakiwa atambue kwanza kisha ndio atende. Anatakiwa ajifunze dini yake na atende kwa ujuzi na Allaah ndiye anajua zaidi.

[1] Ni yule Imaam mwenye kujulikana mmoja katika wale wanachuoni wakubwa na wale maimamu wane. Anaitwa Muhammad bin Idriys ash-Shaafi´iy al-Matwlabiy. Alizaliwa 150 na akafariki 204.

[2] Abu ´Abdillaah Muhammad bin Ismaa´iyl bin Ibraahiym al-Bukhaariy. Anatoka Bukhaaraa mashariki ya kati. Amezaliwa 194 na akafariki 256. Alikuwa na miaka 62. Yeye ndiye mwandishi wa “as-Swahiyh” na vitabu vingine vikubwa na vyenye manufaa.

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 11-12
  • Imechapishwa: 15/10/2016