07. Faida na thawabu za kuifundisha na kusambaza elimu

Unapowafundisha wengine elimu na ukaisambaza kwa watu unalipwa thawabu kwa njia nyingi:

1 – Kueneza kwako elimu unaeneza dini ya Allaah (´Azza wa Jall). Hivyo unakuwa katika wapambanaji jihaad katika njia ya Allaah, kwani unazifungua nyoyo kwa elimu kama ambavyo wapiganaji jihaad wanaifungua miji kwa silaha na imani.

2 – Miongoni mwa baraka za kueneza elimu na kuifundisha ndani yake kuna kuihifadhi na kuilinda Shari´ah ya Allaah (´Azza wa Jall), kwa sababu Shari´ah haihifadhiki bila ya elimu.

3 – Miongoni mwa baraka za kueneza elimu ni kwamba unamtendea wema huyu ambaye umemfunza, kwa sababu unamfanya kuifahamu dini ya Allaah (´Azza wa Jall). Akimwabudu Allaah kwa ujuzi basi unalipwa sawa na thawabu zake, kwa sababu wewe ndiye ambaye umemwongoza katika kheri hiyo. Mwenye kuongoza katika kheri ni kama mwenye kuitenda.

4 – Kueneza elimu na kuifundisha kunaifanya inazidi. Elimu ya mwanachuoni inazidi akiwasomesha watu. Kwa sababu ni kujikumbusha yale aliyohifadhi na kuyafungua yale ambayo hakuyahifadhi. Kama alivosema msemaji:

يزيد بكثرة الإنفاق منه

Inazidi kwa kuitoa kwa wingi

وينقص إن به كفا شددتا

Na inapungua kwa kuizuia

Bi maana inapungua kwa kule kuizuia na kutoifunza.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Du´aa´ al-Qunuut-il-Witr, uk. 12-13
  • Imechapishwa: 09/03/2024