06. Allaah anapokutunuku kitu na asikubarikie nacho

Unibariki katika kile Ulichotoa – Baraka ni kheri  nyingi na zenye kudumu. Maana yake  ni kwamba niteremshie baraka katika kile Ulichonipa.

“… katika kile Ulichotoa.”

Kwa maana ya kwamba Ulichonipa katika mali, watoto, elimu na mengineyo anayotoa Allaah (´Azza wa Jall). Kwa hiyo unamuomba Allaah akubarikie vitu hivyo. Kwa sababu Allaah asipokubarikia katika kile anachokupa basi umekosa kheri nyingi. Wako watu  wengi ambao wamepewa mali nyingi lakini wanahesabiwa ni miongoni mwa mafukara, kwa sababu hawanufaiki na mali yao. Wanaikusanya lakini hawanufaiki nayo, jambo ambalo ni kuondolewa baraka. Watu wengi wanakuwa na watoto, hata hivyo hawanufaiki nao kwa sababu wanakuwa ni wenye kuwaasi. Watu hawa hawakubarikiwa katika watoto wao. Utawakuta baadhi ya watu wamepewa elimu nyingi, lakini wanakuwa ni sawa na wasiokuwa wasomi. Haionekani athari ya elimu yao katika ´ibaadah zao, maadili yao, tabia zao na wala katika kuamiliana kwao na watu. Bali elimu hiyo inaweza kumpelekea kuwafanyia kiburi waja wa Allaah, kujikweza kwao na kuwadharau. Mtu huyu hajui kuwa Allaah ndiye ambaye amemtunuku elimu hiyo. Utamkuta watu hawakunufaika na elimu yake; si kwa kufundisha, kutoa miongozo wala kwa kutunga vitabu. Bali ni elimu iliyoishilia kwake mwenyewe. Hapana shaka kwamba huku ni kunyimwa kukubwa. Ingawa elimu ndio kitu kikubwa cha baraka ambacho Allaah anampa mja.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Du´aa´ al-Qunuut-il-Witr, uk. 10-12
  • Imechapishwa: 09/03/2024