07. Fadhilah za Abu Bakr, ´Umar na ´Uthmaan

29 – ´Ubaydullaah bin Sa´d bin Ibraahiym bin Sa´d ametukhabarisha: Ami yangu ametuhadithia: Baba yangu amenikhabarisha, kutoka kwa Swaalih, kutoka kwa Abuz-Zinaad, ambaye amesimulia kwamba Abu Salamah bin ´Abdir-Rahmaan bin ´Awf amemukhabarisha, ambaye amesimulia kuwa ´Abdur-Rahmaan bin Naafiy´ bin ´Abdil-Haarith al-Khuzaa´iy amemukhabarisha, ambaye ameeleza kuwa Abu Muusa al-Ash´ariy amemukhabarisha:

”Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa amekaa kwenye bustani yenye kisima kilichopinda Madiynah huku amenyoosha miguu yake. Abu Bakr akabisha hodi ambapo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akamwambia: ”Mwache aingie na mpe bishara ya Pepo.” Akafanya hivo na Abu Bakr akaingia ndani ambapo akanyoosha miguu yake. Kisha ´Umar akabisha hodi ambapo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akamwambia: ”Mwache aingie na mpe bishara ya Pepo.” Akafanya hivo.” Kisha ´Uthmaan akabisha hodi ambapo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akamwambia: ”Mwache aingie na mpe bishara ya Pepo – atafikwa na mitihani.”[1]

30 – ´Aliy bin Hujr amemukhabarisha: Ismaa´iyl amemukhabarisha, kutoka kwa Muhammad bin ´Amr, kutoka kwa Abu Salamah, kutoka kwa Naafiy´ bin ´Abdil-Haarith al-Khuzaa´iy:

”Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliingia bustani moja wapo ya Madiynah na kumwambia Bilaal: ”Nishikie mlango.” Abu Bakr akaja na kuomba idhini ya kuingia ndani. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa amekaa kwenye kisima kilchopinda hali ya kunyoosha miguu yake. Bilaal akaja na kusema: ”Abu Bakr huyu hapa anaomba idhini ya kuingia ndani. Akasema: ”Mwache aingie na mpe bishara ya Pepo.” Akaja na kukaa naye kwenye kisima kilichopinda na akanyoosha miguu yake. Mlango ukabishwa tena. Bilaal akaja na kusema: ”´Umar huyu hapa anaomba idhini ya kuingia ndani. Akasema: ”Mwache aingie na mpe bishara ya Pepo.” Akaja na kukaa naye kwenye kisima kilichopinda na akanyoosha miguu yake. Mlango ukabishwa tena. Bilaal akaja na kusema: ”´Uthmaan huyu hapa anaomba idhini ya kuingia ndani. Akasema: ”Mwache aingie na mpe bishara ya Pepo na pia atafikwa na mtihani.”

31 – ´Ubaydullaah bin Sa´iyd na Muhammad bin al-Muthannaa, na tamko ni lake,  wametukhabarisha, kutoka kwa Yahyaa, kutoka kwa ´Uthmaan bin Ghiyaath, kutoka kwa Abu ´Uthmaan, kutoka kwa Abu Muusa al-Ash´ariy, ambaye amesema:

”Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa kwenye bustani wakati ambapo bwana mmoja aliomba idhini ya kuingia ndani, ambapo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: ”Mfungulieni mlango na mumpe bishara ya Pepo. Nikamfungulia na kumpa bishara ya Pepo.” Alikuwa ni Abu Bakr. Kisha mtu mwingine akaomba idhini ya kuindia ndani, ambapo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: ”Mfungulieni mlango na mumpe bishara ya Pepo. Alikuwa ni ´Umar. Halafu mtu mwingine akaomba idhini ya kuindia ndani, ambapo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: ”Mfungulieni mlango na mumpe bishara ya Pepo kutokana na mtihani.” Nikamfungulia na nikampa bishara ya Pepo na nikamweleza yale aliyosema. Akasema: ”Allaah ndiye anayetakwa msaada.”

32 – ´Ubaydullaah bin Sa´iyd amemukhabarisha: Yahyaa amemukhabarisha: Ibn Abiy ´Aruubah ametuhadithia: ´Amr bin ´Aliy amemukhabarisha: Yaziyd – Ibn Abiy Zuray´ –na Yahyaa amemukhabarisha: Sa´iyd ametuhadithia, kutoka kwa Qataadah, kutoka kwa Anas, ambaye amesimulia:

”Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipanda Uhud akiwa pamoja na Abu Bakr, ´Umar na ´Uthmaan. Ndipo ukaanza kutikisika ambapo akaupiga mguu wake na kusema: ”Tulia! Mtume, mkweli na mashahidi wawili.”[2]

Tamko ni la ´Amr.

33 – Muhammad bin Bashshaar amemukhabarisha: Muhammad bin ´Abdillaah ametuhadithia: Ash´ath ametuhadithia, kutoka kwa al-Hasan, kutoka kwa Abu Bakrah, ambaye ameeleza kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alisema siku moja:

”Ni nani kati yenu ameota ndoto?” Bwana mmoja akasema: ”Nimeota mizani ikishuka kutoka mbinguni. Ukapimwa uzani wewe na Abu Bakr na ukamshinda uzani Abu Bakr. Kisha akapimwa uzani ´Umar na Abu Bakr na Abu Bakr akamshinda uzani. Kisha ´Umar akapimwa uzani na ´Uthmaan na ´Umar akamshinda uzani. Kisha mizani ikapandishwa juu.” Nikaona kuchukizwa usoni mwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).”[3]

[1] Ahmad (4/393), al-Bukhaariy (3693) na Muslim (2403).

[2] al-Bukhaariy (3675).

[3] Abu Daawuud (4634), at-Tirmidhiy (2287) na Ahmad (20445). Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika “Swahiyh Sunan at-Tirmidhiy” (4634).

  • Muhusika: Imaam Ahmad bin Shu´ayb an-Nasaa’iy (afk. 303)
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fadhwaa-il-us-Swahaabah, uk. 44-46
  • Imechapishwa: 06/09/2026

Turn on/off menu