Yale aliyonakili kutoka kwa Ahmad (Radhiya Allaahu ´anh) ya kwamba Lafdhwiyyah ni Jahmiyyah, yamesihi kutoka kwake. Amesema hivo kwa sababu Jahm na wafuasi wake wametamka waziwazi ya kwamba Qur-aan ni kiumbe, na wale waliosema kuwa matamshi ya Qur-aan yameumbwa wamejificha nyuma ya nadharia ili baadaye waseme kuwa Qur-aan ni kiumbe. Kipindi hicho waliwaogopa Ahl-us-Sunnah kutamka waziwazi kwamba Qur-aan ni kiumbe, matokeo yake ndipo wakasema kuwa matamshi ya Qur-aan ni kiumbe. Malengo yao kwa nadharia hiyo ni kufikia kusema kwamba Qur-aan, kwa matamshi yetu, ni kiumbe. Ndio maana Ahmad (Rahimahu Allaah) akawaita kuwa ni Jahmiyyah. Amesema tena kuwa Lafdhwiyyah ni waovu zaidi kuliko Jahmiyyah[1].

Kuhusu yale ambayo Muhammad bin Jariyr alinakili kutoka kwa Ahmad (Rahimahu Allaah) juu ya kwamba yule mwenye kusema kuwa matamshi yake ya Qur-aan hayakuumbwa ni mzushi, alichokusudia ni kuwa Salaf katika Ahl-us-Sunnah kamwe hawakuwahi kuzungumzia jambo hilo. Na wala hawakuhitaji kufanya hivo. Nadharia hiyo ni mambo mepya yenye kutoka kwa watu wenye kuchupa mipaka na wapumbavu waliyokuja na mambo yaliyozuliwa, wakayaingilia yale mambo waliyokatazwa ya upotevu na ´Aqiydah zilizosimangwa na wakapekua yale mambo ambayo hayakupekuliwa na wanazuoni wa Uislamu katika Salaf. Ndipo Imaam Ahmad akasema kuwa nadharia hiyo yenyewe kama yenyewe ni Bid´ah. Sunniy anapaswa kuachana nayo na asiitamke na wala Bid´ah nyenginezo mfano wake zilizozuliwa. Alazimiane na kukomeka na yale yaliyosemwa na wale maimamu wenye kufuatwa katika Salaf, nayo ni kwamba: Qur-aan ni maneno ya Allaah na ambayo hayakuumbwa. Asizidishe juu yake, isipokuwa kumkufurisha yule mwenye kusema kuwa ni kiumbe. Haafidhw Abu ´Abdillaah al-Haakim ametukhabarisha: Abu Bakr Muhammad bin ´Abdullaah al-Jarraahiy ametuhadithia Marw: Yahyaa bin Saasuuyah ametuhadithia: ´Abdul-Kariym as-Sukkariy ametuhadithia: Wahb bin Zam´ah amenikhabarisha: ´Aliy al-Baashaaniy amenikhabarisha: Nimemsikia ´Abdullaah bin al-Mubaarak akisema:

”Mwenye kukufuru herufi moja ya Qur-aan, basi ameikufuru Qur-aan yote. Na mwenye kusema kuwa haamini herufi L/ل, amekufuru.”

[1] as-Sunnah, uk. 29, ya ´Abdullaah bin Ahmad bin Hanbal.

  • Mhusika: Imaam Abu ´Uthmaan Ismaa´iyl bin ´Abdir-Rahmaan as-Swaabuuniy (afk. 449)
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ´Aqiydat-us-Salaf wa Aswhaab-il-Hadiyth, uk. 172-175
  • Imechapishwa: 03/12/2023