05. Qur-aan ni maneno ya Allaah ambayo hayakuumbwa

Nimemsikia Haafidhw al-Haakim Abu ´Abdillaah akisema: Nimemsikia Abul-Waliyd Hassaan bin Muhammad akisema: Nimemsikia Imaam Abu Bakr Muhammad bin Ishaaq bin Khuzaymah akisema:

”Qur-aan ni maneno ya Allaah ambayo hayakuumbwa. Yule mwenye kusema kuwa Qur-aan imeumbwa amemkufuru Allaah Mtukufu. Haukubaliwi ushahidi wake. Hatembelewi akigonjweka. Haswaliwi akifa. Hazikwi kwenye makaburi ya waislamu. Anatakiwa kutakwa atubie na vinginevyo ikatwe shingo yake.”[1]

Kuhusu matamshi ya Qur-aan, Shaykh Abu Bakr al-Ismaa´iyliy al-Jurjaaniy aliandika kwenye barua yake aliyowaandikia watu wa Gilaan:

”Yule mwenye kudai kuwa matamshi yake ya Qur-aan ni kiumbe na huku anaikusudia Qur-aan, basi amesema kuwa Qur-aan imeumbwa.”

Ibn Mahdiy at-Twabariy ameandika katika kitabu chake ”Kitaab-ul-I´tiqaad” ambacho aliwaandikia watu wa mji huo:

”´Aqiydah ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah ni kwamba Qur-aan ni maneno ya Allaah (Subhaanah) ambayo haikuumbwa, wahy, uteremsho, amri na makatazo Yake. Yule mwenye kusema kuwa ni kiumbe ni mwenye kumkufuru Allaah Mtukufu. Qur-aan imehifadhiwa ndani ya vifua vyetu, inasomwa na ndimi zetu na imeandikwa kwenye misahafu yetu. Ni maneno ambayo Allaah (´Azza wa Jall) amezungumza nayo. Yule mwenye kusema kuwa Qur-aan kwa matamshi yake ni kiumbe au kwamba matamshi yake ni kiumbe, ni mjinga mpotevu aliyemkufuru Allaah (´Azza wa Jall).”

Nimetaja kipengele hichi kutoka katika kitabu cha Ibn Mahdiy kwa sababu yamenipendeza na ni yenye kuafikiana na Salaf katika Ahl-ul-Hadiyth. Licha ya kwamba alikuwa na elimu yenye kubobea katika falsafa, ametunga tungo nyingi na alikuwa msitari wa mbele katika wanafalsafa.

Haafidhw Abu ´Abdillaah ametukhabarisha: Nilisoma hati ya mkono ya Abu ´Amr al-Mustamliy: Nimemsikia Abu ´Uthmaan Sa´iyd bin Ishkaab akisema:

”Nilimuuliza Ishaaq bin Ibraahiym kuhusu matamshi ya Qur-aan. Akasema: ”Haitakikani kubishana juu ya hilo. Qur-aan ni maneno ya Allaah na haikuumbwa.”

Muhammad bin Jariyr at-Twabariy (Rahimahu Allaah) amesema katika kitabu chake cha ´Aqiydah alichoandika juu ya maudhui haya:

”Kuhusu matamshi ya waja ya Qur-aan, simjui Swahabah wala mwanafunzi wa Maswahabah yeyote aliyezungumzia hilo – hakuna mwengine aliyezungumzia hilo isipokuwa ambaye katika maoni yake kuna kutosheleza na kukidhi, katika kumfuata kuna busara na uongofu na ambaye maneno yake yanasimama mahali pa maneno ya wale maimamu wa kwanza: Abu ´Abdillaah Ahmad bin Hanbal (Rahimahu Allaah). Abu Ismaa´iyl at-Tirmidhiy (Rahimahu Allaah) amenihadithia: Nimemsikia Abu ´Abdillaah Ahmad bin Hanbal (Rahimahu Allaah) akisema:

”Lafdhwiyyah ni Jahmiyyah. Allaah (´Azza wa Jall) amesema:

وَإِنْ أَحَدٌ مِّنَ الْمُشْرِكِينَ اسْتَجَارَكَ فَأَجِرْهُ حَتَّىٰ يَسْمَعَ كَلَامَ اللَّـهِ

“Endapo mmoja katika washirikina atakuomba umlinde, basi mlinde mpaka aweze kusikia maneno ya Allaah.”[2]

Anayasikia kutoka kwa nani?”

Kisha nikawasikia baadhi ya maswahiba zetu, siwakumbuki majina yao, wakitaja kutoka kwake (Radhiya Allaahu ´anh) ya kwamba amesema:

”Mwenye kusema kuwa matamshi ya Qur-aan yameumbwa ni Jahmiy, na mwenye kusema hayakuumbwa ni mzushi.”

Wala sioni kuwa inafaa kusema kitu kingine kinyume na alichosema, kwa sababu hatuna imamu mwingine tunayemfuata katika suala hilo zaidi yake. Anatosha na kukidhi, ni imamu anayefuatwa. Allaah amrehemu na amuie radhi.”[3]

Hivi ndivo alivosema Muhammad bin Jariyr katika kitabu chake cha ´Aqiydah ambayo nimeyanakili hapa. Hapa Muhammad bin Jariyr anayakana yale yote aliyotuhumiwa na kunasibishiwa katika kupondoka kutokana na Sunnah na kumili katika Bid´ah.

[1] Zayd al-Madkhaliy (Rahimahu Allaah) amesema:

”Si haki ya kila mmoja kusimamisha adhabu za Kishari´ah. Isipokuwa yule aliyetawalia madaraka ya waislamu. Mtawala wa Kiislamu ndiye mwenye haki ya kusimamisha adhabu kama vile ya kumuua anayeua makusudi, anakata mkono wa mwizi, anampiga bakora mzinzi ambaye hajawahi kuingia ndani ya ndoa, atampiga mawe mzinzi ambaye kishawahi kuingia ndani ya ndoa na atampiga mijeledi mtu ambaye anawatuhumu wengine machafu na mnywaji pombe. Wakati mwingine adhabu inaweza kuwa kwa njia ya kuua. Yote haya ni mambo yanayopasa mamlaka. Hakuna mwengine yeyote, hata kama ni mwanachuoni,  anayo haki ya kusimamisha adhabu si juu ya nafsi yake mwenyewe wala waja wengine isipokuwa ikiwa kama ana idhini kutoka kwa mtawala, kwa mfano mahakimu wa kidini na maafisa wa polisi. Hii ndio ´Aqiydah ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah juu ya jambo hili.” (at-Ta´liyqaat al-Latwiyfah ´alaa Usuwl-is-Sunnah al-Muniyfah, uk. 17-18)

[2] 9:6

[3] Swariyh-us-Sunnah, uk. 28-29

  • Mhusika: Imaam Abu ´Uthmaan Ismaa´iyl bin ´Abdir-Rahmaan as-Swaabuuniy (afk. 449)
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ´Aqiydat-us-Salaf wa Aswhaab-il-Hadiyth, uk. 169-172
  • Imechapishwa: 03/12/2023