Ahl-ul-Hadiyth wanaona kuwa Qur-aan ni maneno ya Allaah ambayo hayakuumbwa, Kitabu Chake, ufunuo na uteremsho wake. Yule mwenye kusema kuwa ni kiumbe na akaamini hivo ni kafiri kwa mtazamo wao.

Qur-aan, ambayo ni maneno na wahy wa Allaah, ndio ambayo Jibriyl aliteremka nayo kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam); Qur-aan ya kiarabu kwenda kwa watu wanaojua, hali ya kuwa ni yenye kutoa bishara njema na kuonya. Kama alivosema Allaah (´Azza wa Jall):

وَإِنَّهُ لَتَنزِيلُ رَبِّ الْعَالَمِينَ نَزَلَ بِهِ الرُّوحُ الْأَمِينُ عَلَى قَلْبِكَ لِتَكُونَ مِنَ الْمُنذِرِينَ بِلِسَانٍ عَرَبِيٍّ مُّبِينٍ

“Hakika huu ni uteremsho wa Mola wa walimwengu; ameuteremsha roho mwaminifu [na kuiingiza] kwenye moyo wako ili uwe miongoni mwa waonyaji kwa lugha ya Kiarabu ilio wazi.”[1]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amewafikisha nayo ummah wake, kama alivyoamrishwa katika maneno Yake (Ta´ala):

يَا أَيُّهَا الرَّسُولُ بَلِّغْ مَا أُنزِلَ إِلَيْكَ مِن رَّبِّكَ

“Ee Mtume! Fikisha yale yaliyoteremshwa kwako kutoka kwa Mola wako!”[2]

Yale ambayo (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliyafikisha ni kwa amri ya Allaah (´Azza wa Jall). Vilevile amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

”Je, mnanizuia kufikisha maneno ya Mola wangu?”

Ndio ambayo imehifadhiwa na vifua, inasomwa na ndimi na ikaandikwa ndani ya misahafu. Pasi na kujali namna inavotamkwa, namna inavohifadhiwa na wakati inasomwa, na mahali popote inaposomwa na kuandikwa ndani ya misahafu ya waislamu na vibao vya watoto na maeneo mengine, ni maneno ya Allaah (´Azza wa Jall); inabaki vilevile kuwa ni ile Qur-aan ambayo tunasema kuwa haikuumbwa. Yule mwenye kudai kuwa ni kiumbe amemkufuru Allaah Mtukufu.

[1] 26:192-195

[2] 5:67

  • Mhusika: Imaam Abu ´Uthmaan Ismaa´iyl bin ´Abdir-Rahmaan as-Swaabuuniy (afk. 449)
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ´Aqiydat-us-Salaf wa Aswhaab-il-Hadiyth, uk. 50
  • Imechapishwa: 03/12/2023