06. Sifa mbili za kipekee za mwezi wa Ramadhaan

Hakika Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) ameubagua mwezi wa Ramadhaan miongoni mwa miezi kwa fadhilah nyingi na ameutofautisha kwa sifa nyingi. Amesema (Ta´ala):

شَهْرُ رَمَضَانَ الَّذِي أُنزِلَ فِيهِ الْقُرْآنُ هُدًى لِّلنَّاسِ وَبَيِّنَاتٍ مِّنَ الْهُدَىٰ وَالْفُرْقَانِ ۚ فَمَن شَهِدَ مِنكُمُ الشَّهْرَ فَلْيَصُمْهُ ۖ وَمَن كَانَ مَرِيضًا أَوْ عَلَىٰ سَفَرٍ فَعِدَّةٌ مِّنْ أَيَّامٍ أُخَرَ

“Mwezi wa Ramadhaan ambao [kumeanzwa] kuteremshwa humo Qur-aan ili iwe mwongozo kwa watu na hoja bayana za mwongozo na pambanuo [la haki na ubatilifu]. Basi atakayeshuhudia miongoni mwenu mwezi [mpya] na afunge  swawm. Na atakayekuwa mgonjwa au safarini basi [atimize] idadi katika siku nyinginezo.”[1]

Katika Aayah hii Tukufu Allaah ameutaja mwezi wa Ramadhaan kwa sifa mbili kubwa:

1 – Kushushwa kwa kuteremshwa Qur-aan ndani yake kwa ajili ya kuwaongoza watu kutoka gizani katika kwenye nuru na kuwabainishia haki na batili kupitia Kitabu hiki kikubwa kilichobeba manufaa ya wanadamu, mafanikio yao na furaha yao ulimwenguni na Aakhirah.

2 – Kuwajibishwa swawm yake juu ya ummah wa Muhammad, kwa kuwa Allaah ameamrisha hilo pale aliposema:

فَمَن شَهِدَ مِنكُمُ الشَّهْرَ فَلْيَصُمْهُ

“Basi atakayeshuhudia miongoni mwenu mwezi [mpya] na afunge  swawm.”[2]

Kufunga Ramadhaan ni moja ya nguzo za Uislamu na ni faradhi miongoni mwa faradhi za Allaah, jambo linalojulikana vyema kabisa na kwa maafikiano ya waislamu. Anayeikanusha amekufuru. Atakayekuwa yupo na mwenye afya, basi ni wajibu juu yake kufunga mwezi kwa utekelezaji. Allaah (Ta´ala):

فَمَن شَهِدَ مِنكُمُ الشَّهْرَ فَلْيَصُمْهُ

“Basi atakayeshuhudia miongoni mwenu mwezi [mpya] na afunge  swawm.”

Ikabainika kwamba hakuna budi ya kufunga mwezi, ama kwa utekelezaji au kwa kulipa, isipokuwa kwa mzee aliyefikia uzeeni mkubwa na mgonjwa mwenye maradhi sugu ambao hawawezi kufunga kwa kutekeleza wala kulipa. Hao wana hukumu nyingine itakayokuja kubainishwa – Allaah akitaka.

[1] 02:185

[2] 02:185

  • Muhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ithaaf Ahl-il-Iymaan bi Duruus Shahri Ramadhwaan, uk. 15-16
  • Imechapishwa: 26/01/2026