06. Shirki ambayo Mitume walivutana na watu wake kwa ajili yake

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Ukielewa yale niliyokwambia na moyo wako ukakinaika na ukajua kumshirikisha Allaah ambako Allaah amekuzungumzia kwa kusema:

إِنَّ اللَّـهَ لَا يَغْفِرُ أَن يُشْرَكَ بِهِ وَيَغْفِرُ مَا دُونَ ذَٰلِكَ لِمَن يَشَاءُ

 “Hakika Allaah hasamehi kushirikishwa na kitu chochote na anasamehe yaliyo chini ya hayo kwa Amtakae.” (an-Nisaa´ 04 : 48)

na umeilewa dini ya Allaah ambayo amewatuma kwa ajili yake Mitume, kuanzia wa mwanzo wao mpaka wa mwisho wao, ambayo ndio dini ya kipekee ambayo Allaah anaikubali kutoka kwa mtu, na ukajua jambo lililowapitikia watu wengi kwa kuwa wajinga juu ya hili, hapo utapata faida mbili:

1 – Faida ya kwanza: Ni kufurahi kwa fadhila za Allaah na kwa rahmah Zake. Kama alivyosema Allaah (Ta´ala):

قُلْ بِفَضْلِ اللَّـهِ وَبِرَحْمَتِهِ فَبِذَٰلِكَ فَلْيَفْرَحُوا هُوَ خَيْرٌ مِّمَّا يَجْمَعُونَ

“Sema: “Kwa fadhilah za Allaah na kwa rehema Zake, basi kwa hayo wafurahi. Hayo ni kheri kuliko wanayoyakusanya.” (Yuunus 10 : 58)

2 – Faida ya pili: Umefaidika pia kuwa na khofu kubwa. Ukitambua ya kwamba mtu anaweza kukufuru kwa neno analolitoa mdomoni mwake, na pengine amelisema na huku ni mjinga – lakini hapewi udhuru kwa ujinga – na huenda amelisema na huku akidhani ya kwamba yanamkurubisha kwa Allaah, kama walivyokuwa wakidhani washirikina, na khaswa Allaah akikuongoza kwa yale Aliyoelezea kuhusu watu wa Muusa – pamoja na wema wao na elimu yao – walipomuendea na kumwambia:

اجْعَل لَّنَا إِلَهًا كَمَا لَهُمْ آلِهَةٌ

“Tufanyie mungu kama ambavyo wao wako na miungu!” (al-A´raaf 07: 138)

hapo ndipo khofu na bidii yako itaongezeka kwa yale yatakayokuokoa kutokana na haya na mfano wake.

MAELEZO

Ukielewa… – Bi maana ukielewa yale niliyokwambia kuhusu washirikina wa kale na kwamba walikuwa wakitambua kuwa Allaah ndiye Muumba, Mwenye kuruzuku, Mwenye kuyaendesha mambo, Mwenye kuhuisha na Mwenye kufisha na kwamba walikuwa wakiyaabudu masanamu, mizimu, miti, Malaika na Mitume kwa kuonelea kwamba watawaombea na kuwakurubisha kwa Allaah. Si kwamba waliwaabudu kwa sababu eti wanaumba na wanaruzuku. Walikuwa ni wenye kutambua kuwa Allaah ndiye Muumba, Mwenye kuruzuku, Mwenye kuhuisha, Mwenye kufisha na Mwenye kuyaendesha mambo. Lakini hata hivyo walikuwa wakiwaabudu Malaika, Mitume, masanamu kama mfano wa al-Laat na al-´Uzzaa kwa sababu walikuwa wakiona kuwa wanaweza kuwaombea mbele ya Allaah na kwamba wanawakurubisha mbele ya Allaah. Pamoja na haya yote Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliwapiga vita na akaihalalisha damu na mali yao mpaka wamtakasie ´ibaadah Allaah pekee.

Na moyo wako ukakinaika na ukajua… – Bi maana ukijua shirki ambayo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipigana kwa ajili yake na kwamba inahusiana na kumtekelezea ´ibaadah mwingine asiyekuwa Allaah. Mfano wa ´ibaadah hizo ni nadhiri, kuomba uokozi kwa asiyekuwa Allaah. Hii ndio shirki ambayo ndio dhambi kubwa. Kile kitendo cha mtu kuomba uokozi kwa mti, sanamu, Malaika, Mitume, wafu au nyota ndio shirki. Kwa njia ya kwamba mtu akaomba uokozi kwayo, akaviwekea nadhiri, akawachinjia, akawaomba, akawasujudia na mfano wa matendo kama hayo. Hii ndio dhambi kubwa. Amesema (Ta´ala) kuhusu shirki:

إِنَّ اللَّـهَ لَا يَغْفِرُ أَن يُشْرَكَ بِهِ وَيَغْفِرُ مَا دُونَ ذَٰلِكَ لِمَن يَشَاءُ

“Hakika Allaah hasamehi kushirikishwa na anasamehe yaliyo chini ya hayo kwa amtakae.”[1]

وَلَوْ أَشْرَكُوا لَحَبِطَ عَنْهُم مَّا كَانُوا يَعْمَلُونَ

“Lau wangemshirikisha bila shaka yangeporomoka yale waliyokuwa wakitenda.”[2]

وَلَقَدْ أُوحِيَ إِلَيْكَ وَإِلَى الَّذِينَ مِن قَبْلِكَ لَئِنْ أَشْرَكْتَ لَيَحْبَطَنَّ عَمَلُكَ وَلَتَكُونَنَّ مِنَ الْخَاسِرِينَ

“Hakika umefunuliwa Wahy na kwa wale walio kabla yako kwamba: “Ukifanya shirki bila shaka yataporomoka matendo yako na hakika utakuwa miongoni mwa waliokhasirika.”[3]

Umeielewa dini ya Allaah… – Umeielewa dini ya Uislamu ambayo Allaah amewatumiliza Mitume na akateremsha Vitabu. Inahusiana na kumpwekesha Allaah, kumtakasia Yeye nia, kutii maamrisho Yake na kujiepusha na makatazo Yake. Hii ndio dini ya Uislamu ambayo amesema (Subhaanah):

إِنَّ الدِّينَ عِندَ اللَّـهِ الْإِسْلَامُ

”Hakika dini mbele ya Allaah ni Uislamu.”[4]

Dini ya Uislamu inahusiana na kumpwekesha Allaah, kumtakasia Yeye nia na kujiepusha na shirki, kutii maamrisho Yake, kujiepusha na makatazo Yake. Hii ndio dini ya Uislamu. Dini ya Uislamu sio kufuata kibubusa na kulingania katika Uislamu pasi na kujali ´Aqiydah. Dini ya Uislamu inahusiana na ´Aqiydah na matendo. Inahusu maneno na vitendo. Unatakiwa kuitambua dini ya Allaah kwamba ni kumpwekesha Allaah, kumtakasia Yeye nia, kumwamini Yeye, Mitume Wake, kuamini yale yote aliyokhabarisha Allaah na Mtume Wake kuhusiana na jambo la Pepo, Moto na vyenginevyo. Sambamba na hilo mtu amsadikishe Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kumfuata. Huu ndio Uislamu pamoja pia na kutii maamrisho Yake na kujiepusha na makatazo Yake. Hii ndio dini ya Allaah ambayo wameijahili wengi pamoja na kwamba wanadai kuwa ni ´waislamu` na huku utawaona wanaabudu miti, mawe, masanamu na mawalii. Yote haya ni kutokana na ujinga wao.

Kadhaika umeelewa kuwa mtu anaweza kukufuru kwa neno moja tu linalomtoka mdomoni mwake. Huenda amelisema na huku ni mjinga. Huenda amesema na huku akidhani kuwa linamkurubisha mbele ya Allaah. Inaweza kuwa inahusiana na mtu kuitukana dini au kuichezea shere dini. Matokeo yake akakufuru pasi na kujua. Mtu akamtukana Allaah, akamtukana Mtume, akaifanyia utani dini, akapinga yale aliyowajibisha Allaah au akapinga baadhi ya yale aliyoharamisha Allaah. Matokeo yake anakufuru kwa hayo ilihali hajali na wala hazinduki. Ukiyajua hayo basi utatambua kuwa Allaah amekupa faida mbili kubwa:

[1] 04:48

[2] 06:88

[3] 39:65

[4] 03:19

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Kashf-ish-Shubuhaat, uk. 21-23
  • Imechapishwa: 12/10/2021