Shaykh-ul-Islaam na Imaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Sharti ya tatu ni kupambanua (Tamyiyz) na kinyume chake ni utoto. Mpaka wake ni miaka saba. Hapo ndipo ataamrishwa kuswali, kutokana na kauli ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Waamrisheni watoto wenu kuswali wanapofikisha miaka saba, wapigeni wanapofikisha miaka kumi na watenganishe baina yao katika malazi.”[1]

MAELEZO

Manneo yake:

“Sharti ya tatu… “

Miongoni mwa sharti za kusihi kwa swalah ni uwezo wa kupambanua. Maneno yake:

“… na kinyume chake ni utoto.”

Mtoto mdogo ambaye hajafikisha miaka ya kupambanua ´ibaadah si zenye kumuwajibikia na wala swalah hazisihi kwake. Maneno yake:

“Mpaka wake ni miaka saba.”

Kwa hivyo mtu asipupie kumleta mwanae wa miaka mitatu au miaka minne msikitini kwa lengo la kumzoweza swalah. Wakati wa mazoezi ni miaka saba. Kwa hivyo hakuna haja ya kumleta kwa lengo la mazoezi. Lakini akiletwa basi amweke pambazoni mwake akiwa hamuudhi yeyote na wala hachezicheza. Hakuna neno katika hali hiyo. al-Hasan alimpandia Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wakati alipokuwa katika sujudu.

Maneno yake:

“Hapo ndipo ataamrishwa kuswali.”

Kabla ya miaka saba haamrishwi swalah. Mtoto wa miaka mine, tano au sita haamrishwi swalah. Kipindi hicho ndipo anazowezwa swalah. Mpaka pale anapobaleghe basi anakuwa amekwishaizowea na inakuwa nyepesi kwake. Lakini akiachwa na asiamrishwe mpaka pale atakapobaleghe basi inakuwa nzito, gumu na yenye kumtia tabu. Aidha pengine wakati huo asiwakubalie wazazi wake. Maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Waamrisheni watoto wenu kuswali wanapofikisha miaka saba, wapigeni wanapofikisha miaka kumi na watenganishe baina yao katika malazi.”

Wazazi wanatakiwa kumwamrisha swalah mtoto wao wa miaka saba. Anapofikisha miaka saba basi wanatakiwa kumpiga kipigo cha kumuadabisha na kumfunza. Haitakiwi iwe kipigo cha madhara, kumuumiza mwili au kuvunja kiungo. Bali inatakiwa iwe kipigo chepesi cha kumfanya ahisi kuwa yuko nyuma juu ya faradhi hii tukufu.

[1] Abu Daawuud (495) na Ahmad (6756). Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”al-Irwaa’” (1/266).

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajihiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Shuruwt-is-Swalaah, uk. 15-16
  • Imechapishwa: 13/06/2022