Himdi zote njema anastahiki Allaah. Swalah na amani zimwendee Mtume wa Allaah, kizazi chake na Maswahabah zake wote.

Ama baada ya hayo;

Allaah (Ta´alaa) ameufanya maalum mwezi wa Ramadhaan juu ya miezi mingine kwa heshima na utukufu, akateremsha humo Qur-aan tukufu, kukafaradhishwa humo kufunga kwa ajili ya kushukuru neema hii na akafanya swawm yake ni moja miongoni mwa nguzo zake ambayo hausimami isipokuwa kwazo. Aidha Mtume wetu mtukutu (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasunisha kusimama usiku. Ni mwezi wenye baraka na kheri mbalimbali. Ni mwezi wa kuitikiwa du´aa. Ni mwezi wa kujitolea kipaumbele. Ni mwezi ambao mema yanalipwa maradufu. Mwezi wa fadhilah mbalimbali. Ni mwezi ambao kuna watu wanaachwa huru na Moto. Ni mwezi ambao haulingani na nyakati za miezi mingine. Allaah (Ta´ala) amesema:

شَهْرُ رَمَضَانَ الَّذِي أُنزِلَ فِيهِ الْقُرْآنُ هُدًى لِّلنَّاسِ وَبَيِّنَاتٍ مِّنَ الْهُدَىٰ وَالْفُرْقَانِ ۚ فَمَن شَهِدَ مِنكُمُ الشَّهْرَ فَلْيَصُمْهُ ۖ وَمَن كَانَ مَرِيضًا أَوْ عَلَىٰ سَفَرٍ فَعِدَّةٌ مِّنْ أَيَّامٍ أُخَرَ ۗ يُرِيدُ اللَّـهُ بِكُمُ الْيُسْرَ وَلَا يُرِيدُ بِكُمُ الْعُسْرَ وَلِتُكْمِلُوا الْعِدَّةَ وَلِتُكَبِّرُوا اللَّـهَ عَلَىٰ مَا هَدَاكُمْ وَلَعَلَّكُمْ تَشْكُرُونَ

“Mwezi wa Ramadhaan ambao [kumeanzwa] kuteremshwa humo Qur-aan ili iwe mwongozo kwa watu na hoja bayana za mwongozo na pambanuo [la haki na ubatilifu]. Basi atakayeshuhudia miongoni mwenu mwezi [mpya] na afunge  swawm. Na atakayekuwa mgonjwa au safarini basi [atimize] idadi katika siku nyinginezo. Allaah Anakutakieni mepesi na wala Hakutakieni magumu. [Fungeni siku mlizowekewa] ili mkamilishe idadi na ili mumkabiri Allaah kwa kuwa Amekuongozeni na mpate kushukuru.”[1]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Uislamu umejengwa juu ya mambo matano: kushuhudia ya kwamba hapana mungu wa kweli isipokuwa Allaah na kwamba Muhammad ni Mtume wa Allaah, kusimamisha swalah, kutoa zakaah, kuhiji na kufunga Ramadhaan.”[2]

Katika Hadiyth ya Jibriyl inayotambulika[3] amefasiri (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) Uislamu kwa mambo haya matano. Kutokana na dalili hizi na nyenginezo zilizo na maana yake inapata kutambulika kuwa hausihi Uislamu wa ambaye hafungi mwezi wa Ramadhaan hali ya kukanusha uwajibu wake na kwamba anayeacha kufunga kwa makusudi hazingatiwi kuwa ni muislamu.

Imepokelewa kwamba ambaye atakula siku moja tu ya Ramadhaan pasi na ruhusa, basi siku hiyo haitofidiwa na swawm ya mwaka mzima akifunga. Amepokea Ahmad, Abu Daawuud na al-Bukhaariy kwa cheni ya wapokezi pungufu na wengineo:

“Yule mwenye kula siku moja ya Ramadhaan pasi na ruhusa wala maradhi, basi haiwezi kulipwa na swawm ya mwaka mzima hata akiifunga.”[4]

Ambaye atafunga hali ya kutoridhia, kuchukia, anaona ugumu kufunga, hataki kwenda kinyume na wengine, amezaliwa kati ya wanaoifunga au anafunga kwa sababu ya kuwaona wazazi wamefunga, basi anakosa thawabu nyingi. Kwa sababu hakuleta sharti ya kusamehewa:

“Yule mwenye kufunga Ramadhaan hali ya kuwa na imani na matarajio, basi atasamehewa madhambi yake yaliyotangulia.”[5]

Kuna maafikiano juu yake.

Swalah na amani zimwendee Mtume wetu Muhammad, kizazi chake na Maswahabah zake wote.

[1] 02:185

[2] al-Bukhaariy (08) na Muslim (16).

[3] al-Bukhaariy (50) na Muslim (08).

[4] Abu Daawuud (2396) na at-Tirmidhiy (1723).

[5] al-Bukhaariy (38) na Muslim (760).

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajihiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Duruus fiy Ramadhwaan, uk. 19-20
  • Imechapishwa: 12/04/2023